1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge lapitisha bajeti licha ya utata wa bomba la gesi Tanzania

26 Mei 2013

Licha ya utata na machafuko yaliyozuka kutokana na mpango wa serikali ya Tanzania kujenga bomba la gesi kutoka Mtwara Dar es Salaam, bunge la nchi hiyo limepitisha bajeti ya wizara ya madini na nishati.

Sospeter Muhongo, Minister für Energie und Mineralien in seinem Büro *** Bilder Deutsche Welle, Julia Hahn, November 2012 Ort: Ministry of Energy and Minerals, Daressalam, Tansania *** http://en.wikipedia.org/wiki/North_Mara_Gold_Mine North Mara Gold Mine is an open pit gold mine in the Tarime District of the Mara Region of Tanzania. It is operated by African Barrick Gold. It is one of four gold mines African Barrick Gold, a subsidiary of Barrick Gold, operates in Tanzania, the other three being Tulawaka, Bulyanhulu and the Buzwagi Gold Mine. In the financial year 2009, the four operations produced a combined amount of 716,000 attributable ounces of gold.
North Mara Gold Mine in Tansania Sospeter Muhongo Minister für EnergiePicha: DW/J. Hahn

Shirika la habari la Reuters limeripoti kwamba kwa kupitisha bajeti hiyo, bunge la Tanzania limeamua kuwa mradi huo unaofadhiliwa na China kwa gharama ya dola bilioni 1.2 uendelee kama ulivyopangwa, licha ya maandamano dhidi yake, ambayo yamesababisha watu wawili kupoteza maisha na mali kadhaa kuharibiwa.

Bunge hilo lilikuwa liipitishe bajeti hiyo ya mwaka 2013/2014 siku ya Jumatano, lakini ghasia zilizozuka juu ya mradi huo wa bomba la gesi zililazimisha bunge kusitisha shughuli zake kwa muda. Hatimaye, siku ya Jumamosi (tarehe 25 Mei), wabunge waliipitisha bajeti na kusema kwamba kazi ya ujenzi wa bomba hilo ingeliendelea hadi kukamilika kwake mwezi Disemba 2014.

"Yeyote anayepinga bomba hili si mwenzetu," Waziri wa Nishati a Madini, Sospeter Muhongo, alitangaza bungeni.

Matumaini ya gesi kuinua uchumi

Tanzania inakisia kwamba ina kiwango cha ujazo wa triolioni 41.7 cha gesi kwenye akiba yake. Utafiti kwenye maeneo ya pwani za Tanzania na Msumbiji yameonesha kwamba eneo hilo linaweza kuwa msafirishaji wa tatu kwa ukubwa wa gesi asilia duniani.

Rais Xi Jinping wa China (kushoto) akikaribishwa na Rais Jakaya Kikwete nchini Tanzania.Picha: Reuters

Hata hivyo, wakaazi wa mkoa wa kusini wa Mtwara wanapingana na ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilomita 532, unaofadhiliwa kwa mkopo wa China, hadi wapate sehemu kubwa ya mapato yanayotokana na uendelezaji wa gesi hiyo.

Mkuu wa polisi wa mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa, aliiambia Reuters kwamba watu watatu waliuawa kwenye ghasia za Jumatano na Alhamisi mkoani humo, ambapo pia watu 121 wametiwa mbaroni.

Siku ya Jumamosi, bunge liliteua kamati ya kuchunguza sababu za ghasia hizo na kutoa mapendekezo ya kukabiliana na vurugu za mara kwa mara dhidi ya mradi huo wa bomba la gesi wa serikali.

Muhongo alisisitiza kwamba serikali ingeliendelea na ujenzi wake licha ya upinzani wa wananchi, akisema kwamba mradi huo utasaidia kuinua uchumi wa Tanzania kufikia asilimia 8 mwaka 2015 kutoka asilimia 6.9 mwaka 2012. "Njia pekee ya kuuinua uchumi wetu ni kujenga bomba hili... bomba hili litaondosha umasikini nchini mwetu," alisema.

Mageuzi ya shirika la umeme

Waziri huyo pia alisema kwamba mageuzi kwenye Shirika la Umeme la nchi hiyo, TANESCO, yatagharimu dola milioni 500, yakijumuisha ulipaji wa madeni ya nje.

Jeshi la Polisi nchini Tanzania likikabiliana na wananchi kutuliza ghasia.Picha: AP

"Benki ya Dunia itatupa dola milioni 300 na tumepokea mkopo wa dola milioni 200 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa kulifanyia mageuzi shirika la TANESCO," alisema akiongeza kwamba serikali itapitia mapendekezo mbalimbali juu ya marekebisho ya shirika hilo pekee la umeme nchini Tanzania.

Hivi karibuni, serikali ilisema kuwa inafikiria kuligawa shirika hilo linaloendeshwa kwa hasara katika sehemu tatu zenye dhamana ya uzalishaji wa umeme, usambazaji na ugawaji.

Sera ya kuhodhi sekta ya umeme imethibitika kutokuwa na manufaa, ambapo ni asilimia 21 tu ya Watanzania wenye huduma hiyo miaka 5o baada ya uhuru, ambao nao hawaupati kwa uhakika wala kwa wakati, alisema Waziri Muhongo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Sekione Kitojo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW