Bunge Marekani laidhinisha msaada kwa Ukraine
5 Juni 2026
Haya yanafanyika wakati ambapo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, amemuandikia barua ya wazi Rais wa Urusi Vladimir Putin akitaka mazungumzo ya amani ya ana kwa ana.
Bunge hilo la Marekani limepitisha mswada huo uliowasilishwa bungenina Wademocrat kwa kura 226 dhidi ya 195 huku karibu ya kura 20 zikitoka kwa chama cha Republican chake Rais Donald Trump.
Hii inamuongezea shinikizo Trump ambaye hivi majuzi alitoa matamshi makali ya kuikosoa Jumuiya ya Kujihami ya NATO na hakuonesha kuiunga mkono Ukraine iliyovamiwa na Urusi kuanzia Februari 2022.
Trump katika njia panda
Mswada huo bado unahitaji kuidhinishwa na seneti kisha utumwe kwake Rais Donald Trump kwa ajili ya kutiwa saini ingawa anaweza kugoma kuusaini.
Kura hiyo inamuweka Trump katika njia panda kwasababu endapo atakataa kuusaini mswada huo basi atakuwa amewapinga baadhi ya Warepublican, kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula ambao chama cha Republican kinapania kutetea wingi wake mdogo katika mabunge yote.
Mswada huo unasema mazungumzo yote ya amani ni sharti yafanyike kwa kuzingatiwa uhuru wa Ukraine na yasifanywe kwa masharti ya Urusi.
Haya yanafanyika wakati ambapo Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Johann Wadephul ametoa wito kwa Rais Vladimir Putin wa Urusi kushiriki mazungumzo yanayolenga kuvimaliza vita vya Ukraine, akidai ni sharti Ulaya ishirikishwe katika makubaliano yoyote yatakayofikiwa.
Akizungumza wakati akiwa ziarani huko Mexico City, Wadephul amesema mgogoro huo umefikia hatua ambayo juhudi za kufikia makubaliano ya kuumaliza ni za dharura.
Matamshi yake yamekuja wakati ambapo Rais Volodymyr Zelenskiy akiwa amechapisha barua ya wazi kwa Rais Putin akitaka wafanye mazungumzo huku juhudi za Marekani za upatanishi zikiwa zimekwama.
Hatari ya ajali ya nyuklia Ulaya
Donald Trump ameikaribisha hatua hiyo ya Zelenskiy.
"Kwa kweli, sijui. Ninafurahi kwamba wanazungumza kuhusu kukutana. Nafikiri tumesaidia sana kuhusiana na hilo. Najua hasa kile unachofanya ila nafikiri itakuwa vyema wakikutana. Wanastahili kuvimaliza vita hivyo," alisema Trump.
Hayo yakijiri Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA, limesema usitishwaji mdogo wa mapigano uliosimamiwa na shirika hilo katika eneo la Zaporizhzhya karibu na kinu cha nyuklia utaanza kutekelezwa hii leo, kutoa nafasi ya ukarabati wa njia kuu ya usambazaji umeme kwenye kinu hicho.
Kinu hicho cha Zaporizhzhya kusini mashariki mwa Ukraine ndicho kikubwa cha nyuklia barani Ulaya na kilitekwa na Urusi muda mfupi baada ya Urusi kuanza uvamizi wake kamili. Kinu hicho kimekuwa kikishambuliwa mara kwa mara katika vita hivyo na kuzua hofu ya ajali ya nyuklia. IAEA inasema huu ni usitishwaji wa sita wa mapigano uliosimamiwa na mkuu wake Rafael Grossi.
Kwengineko mamlaka nchini Ukraine zinasema mashambulizi ya Urusi yamesababisha vifo vya watu 4 katika maeneo kadhaa ya Ukraine.
Vyanzo: DPAE/AFPE