Bunge Sudan kusini larefusha muda wa rais Kiir madarakani
12 Julai 2018Makundi ya upinzani nchini Sudan kusini katika siku za nyuma yalishutumu hatua kama hiyo kuwa inakwenda kinyume na sheria.
Bunge lilipiga kura leo kurefusha muda wa kubakia madarakani kwa rais Salva Kiir kwa muda wa miaka mitatu zaidi, hatua ambayo bila shaka itatatiza juhudi za kuleta amani katika nchi hiyo changa duniani. Mswada wa mabadiliko ya katiba katika kipindi cha mpito nambari tano kwa mwaka 2018 umepitishwa na bunge la taifa," alisema spika wa bunge Anthony Lino Makana baada ya wabunge kwa kauli moja kupiga kura kupitisha mswada huo ambao si lazima utiwe saini kuwa sheria na Kiir.
Sheria hiyo itamruhusu Kiir kubakia madarakani hadi mwaka 2021 hata wakati akiwa anajishughulisha na duru ya hivi karibuni kabisa ya majadiliano ya kimkoa ya amani pamoja na makamu wake wa zamani ambaye hivi sasa ni kiongozi wa waasi Riek Machar katika kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka minne sasa.
Uchaguzi ulikuwa ufanyike mwaka huu, lakini mzozo umesababisha muda wa kufanyika uchaguzi huo kushindikana. Waziri wa sheria Paulino Wanawilla , ambaye aliwasilisha mswada huo, alisema utazuwia serikali kutangazwa kuwa si halali, wakati muda wake wa kuwapo madarakani utakapomalizika.
Kiir na Machar waliingia vitani Desemba 2013.
Tangu wakati huo mamia kwa maelfu ya watu wameuwawa na mamilioni wengine wamelazimika kukia makaazi yao, na kuzusha mzozo mkubwa wa wakimbizi katika kanda hiyo pamoja na kiasi kikubwa cha njaa.
Mazungumzo ya amani
Duru kadhaa za mazungumzo, yaliyosimamiwa na kundi la mataifa yanayofanya biashara ya kanda hiyo linalojulikana kama Intergovernmental Authority on Development , IGAD, ama mamlaka ya ushirikiano wa serikali katika maendeleo, hadi sasa zimeshindwa kuleta amani ama hata makubaliano ya muda mrefu ya kusitisha mapigano.
Mazungumzo ya mwisho yameshuhudia makubaliano mengine ya kusitisha mapigano wakati mapendekezo, ikiwa ni pamoja na kugawana madaraka na Machar kurejea katika wadhifa wake wa makamu wa rais, bado yanajadiliwa.
Wasudan kusini milioni saba, zaidi ya nusu ya idadi jumla ya wakaazi wa nchi hiyo, watahitaji msaada wa chakula katika mwaka huu 2018, kwa mujibu wa Umoja wa mataifa.
Wakati huo huo baraza la Usalama la Umoja wa mataifa linatarajiwa kupiga kura wiki hii kuweka vikwazo vya silaha dhidi ya Sudan kusini, ikiwa ni pendekezo la Marekani ambalo linafuatia makubaliano ya kugawana madaraka baina ya viongozi hao wawili wanaogombana.
Marekani ni mfadhili mkuu wa misaada kwa Sudan kusini, na ilikuwa muungaji mkono mkuu wa uhuru wa nchi hiyo uliopatikana mwaka 2011.
Lakini uvumilivu wa washirika wa kigeni wa Sudan kusini umekwisha baada ya juhudi kadhaa kushindwa kuleta amani nchini humo, ambayo hivi sasa imo katika mwaka wa nne wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyolenga mauaji ya kikabila, ubakaji wa makundi pamoja na madhila mengine yanayotokea.
Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe/rtre
Mhariri: Mohammed Khelef