1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Burkina Faso, Mali zaonya dhidi ya uingiliaji kijeshi Niger

1 Agosti 2023

serikali za kijeshi za Mali na Burkina Faso zimeonya kuwa uingiliaji wowote kijeshi Niger utazingatiwa kuwa "tangazo la vita". Mivutano inaendelea kuongezeka kati ya Niger na mtawala wake wa zamani pamoja na nchi jirani

Coup aftermath in Niger
Waniger waliandamana nje ya ubalozi wa Ufaransa katika mji mkuu NiameyPicha: Souleymane Ag Anara/REUTERS

Wanajeshi hao waasi kupitia Kanali Amadou Abdramane waliishambulia Paris kwenye televisheni ya taifa. "Katika kutekeleza sera yake ya kutafuta njia za kuingilia kijeshi nchini Niger, Ufaransa, kwa ushirikiano wa baadhi ya watu wa Niger, ilifanya mkutano katika makao makuu ya Jeshi la Niger la Ulinzi wa Taifa ili kupata vibali muhimu vya kisiasa na kijeshi." Alisema Abdramane.

Soma pia: Jenerali Abdourahamane Tiane ajitangaza kuwa kiongozi mpya Niger

Ufaransa ilijibu jana usiku huku Waziri wa Mambo ya Kigeni Catherine Colonna akikanusha tuhuma hizo na kuongeza kuwa bado inawezekana kumrejesha Bazoum madarakani.

Kanali Amadou Abdramane akiituhumu UfaransaPicha: ORTN - Télé Sahel/AFP

Rais Emmanuel Macron ameapa kuchukua hatua ya haraka na kali ikiwa raia wa Ufaransa au maslahi yake yatashambuliwa baada ya maelfu ya watu kuandamana nje ya ubalozi wa Ufaransa mjini Niamey. Macron amezungumza mara kadhaa na Bazoum pamoja na viongozi wa kikanda.

Burkina, Mali zaonya dhidi ya uingiliaji Niger

Na katika ishara ya kuongezeka mvutano wa kikanda, serikali za kijeshi za Mali na Burkina Faso zimeonya jana usiku kuwa uingiliaji wowote kijeshi nchini Niger utazingatiwa kuwa "tangazo la vita" pia kwa nchi zao.

Akizungumza kwenye televisheni ya taifa, Kanali Abdoulaye Maiga, Waziri wa Tawala za Mikoa na Ugatuzi wa serikali ya kijeshi ya Mali alionya kuhusu madhara makubwa ya uingiliaji kijeshi nchini Niger, ambayo yanaweza kuidhoofisha kanda nzima. "Serikali za mpito za Burkina Faso na Mali, zimeelezea mshikamano wao wa kidugu na watu wa Mali na Burkina Faso na ndugu zao wa Niger ambao wameamua kwa hiari yao wenyewe kuchukua hatima yao mkononi na kuchukua mamlaka yao."

Kiongozi wa mapinduzi Jenerali Abdourahmane TianiPicha: Balima Boureima/REUTERS

Aidha amesema wanakataa kutekeleza kile walichosema vikwazo haramu vya kikatili dhidi ya watu na maafisa wa Niger.

Bazoum – mshirika wa nchi za Magharibi ambaye alichaguliwa kidemokrasia miaka miwili iliyopita kwa mara ya kwanza tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake aliondolewa madarakani Julai 26 na kikosi chenye nguvu cha Ulinzi wa Rais.

Mkuu wa walinzi wa rais Jenerali Abdourahamane Tiani alijitangaza kiongozi mpya – lakini tangazo hilo limepuuzwa kimataifa na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Afrika Magharibi – ECOWAS imempa wiki moja kukabidhi madaraka kwa Bazoum.

Kamatakamata ya viongozi yaendelea Niger

Tayari watawala hao wa kijeshi wameanza kamatamata ya watu wanaoonekana kumuunga mkono Bazoum. Jumatatu, wanachama 180 wa chama tawala walitiwa mbaroni.

Rais wa Chad Idriss Deby alikutana na Bazoum NiameyPicha: Presidency of Chad/Handout/Anadolu Agency/picture alliance

Waziri wa Nishati Mahamane Sani Mahamadou, Waziri wa Madini Ousseini Hadizatou na rais wa Chama cha Niger cha Demokrasia na Ujamaa – PNDS, Foukamoye Gado, ni miongoni mwa waliokamatwa.

Msemaji wa chama hicho Hamid N'Gade amesema Waziri wa Mambo ya Ndani Hana Amadou Souley, Waziri wa Uchukuzi Oumarou Malam Alma na naibu wake, Kalla Moutari pia walikamatwa na viongozi wa mapinduzi. 

Chama cha Bazoum cha PNDS kimeonya kuwa Niger iko katika hatari ya kuwa utawala wa kidikteta na kimabavu baada ya msururu wa kamatakamata hizo. Umoja wa Ulaya umelaani kukamatwa kwa mawaziri hao na kutaka waachiliwe mara moja.

Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya zimelaani kuondolewa madarakani rais Bazoum, ikiwa ni mapinduzi ya saba ya kijeshi katika chini ya miaka mitatu katika mataifa ya Afrika ya Kati na Magharibi ambayo yamehujumu hatua zilizopigwa za kidemekrasia katika eneo hilo.

afp, ap, reuters, dpa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW