Milio ya bunduki yasikika kwenye kambi za jeshi Burkina Faso
23 Januari 2022Shirika la habari la AFP limeripoti kwamba kulikuwa pia na milio ya risasi kwenye kambi za miji ya kaskazini ya Kaya na Ouahigouya. AFP imesema wakaazi wa miji hiyo wameelezea hayo. Hali hiyo ilizua hofu kwamba huenda kulitokea jaribio la mapinduzi baada ya wiki kadhaa za malalamiko kuhusu serikali inavyoyashughulikia makundi ya waislamu waasi nchini humo.
Serikali ya Burkina Faso, imethibitisha juu ya milio ya risasi kusikika kwenye kambi kadhaa nchini humo lakini imekanusha kutokea mapinduzi ya kijeshi. Wakati huo huo waziri wa ulinzi wa Burkina Faso, Aime Barthelemy Simpore amesema rais Roch Marc Christian Kabore hajazuiliwa kama taarifa za kupotosha zinavyozunguuka.
Mwandishi wa habari AFP ameripoti kwamba polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kutawanya maandamano ya karibu watu 300 waliokusanyika katika eneo la katikati mwa mji mkuu, Ouagadougou kuunga mkono uasi wa wanajeshi.
Milio hiyo ya risasi imesikika siku moja tu baada ya watu waliaoandamana mjini Ouagadougou kumtaka rais Roch Marc Christian Kabore ajiuzulu. Kabore anakabiliwa na upinzani unaozidi kukua tangu alipochaguliwa tena mwezi Novemba mwaka 2020. Amemfuta kazi waziri wake mkuu na mwezi uliopita alibadilisha sehemu kubwa ya baraza la mawaziri.
Vitendo vya askari ni ishara ya kutoridhika
Shirika la utangazaji la serikali RTB limeandika kwenye kichwa cha habari kinachoelezea kuwa milio ya risasi kama ni ishara ya vitendo vya askari kutoridhika lakini uongozi wa kijeshi unafanya kila jitihada kurejesha hali ya utulivu katika kambi husika.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, watu waliozungumza na shirika hilo wamesema milio hiyo ilianza alfajiri na kuendelea hadi mapema asubuhi leo kwenye kambi ya Sangule Lamizana, ambayo ni makao makuu ya maafisa wa jeshi na gereza ambalo baadhi ya wafungwa wake ni askari waliohusika katika jaribio la mapinduzi la mwaka 2015 ambalo halikufanikiwa.
Mapema mwezi huu wanajeshi wanane walikamatwa kutokana na tuhuma za kupanga njama dhidi ya serikali. Mmoja wapo ni Jenerali Gilbert Diendere, aliyekuwa mshirika mkuu wa rais wa zamani wa Burkina Faso Blaise Compaore. Jenerali Diendere sasa anatumikia kifungo cha miaka 20.
Wakati huo huo anakabiliwa mahakamani na tuhuma za kuhusika katika mauaji ya mwaka 1987 ya kiongozi wa mapinduzi nchini humo, Thomas Sankara, aliyeuawa katika maandamano yaliyomwingiza Compaore madarakani. Compaore, alipinduliwa mwaka 2014 na alikimbilia nchini Ivory Coast, na yeye pia anakabiliwa na mashtaka ya mauaji hayo bila ya yeye kuwepo.
Ghasia zinazidi kuongezeka katika taifa hilo la Afrika Magharibi lililokuwa na amani wakati wote. Wakati huo huo mashambulizi yanayohusishwa na makundi ya kigaidi ya al-Qaida na kundi linalojiita dola la IS yanaongezeka. Maelfu ya watu wameuawa nchini Burkina Faso katika miaka ya hivi karibuni na takriban watu milioni 1.5 wamelazimika kuyakimbia makazi yao.
Vyanzo: AP/RTRE/AFP