Burkina Faso yaendelea na maombolezo ya kitaifa
18 Januari 2016Burkina Faso inaendelea na maombolezo ya kitaifa ya siku tatu yaliyoanza jana Jumapili, kuwakumbuka waathirika wa mashambulizi ya kigaidi, wakati ambapo maafisa wamesema idadi ya watu waliouawa katika shambulizi hilo imefikia 29.
Kipindi hicho cha maombolezo kilitangazwa na Rais wa Burkina Faso, Roch Marc Christian Kabore ambaye amesema kwamba usalama umeimarishwa zaidi kwenye mji mkuu, Ouagadougou na kwenye mipaka ya nchi hiyo. Hatua hiyo imefikiwa baada ya wanamgambo wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda kuishambulia hoteli moja na mgahawa ambao unatumiwa zaidi na raia wa kigeni.
''Tayari serikali imepatiwa maagizo ya kuchukua hatua madhubuti kuimarisha usalama kwenye taasisi, maeneo muhimu ya umma na kwenye mipaka na eneo la kuingilia kwenye miji mikubwa ya nchi yetu. Tutayatekeleza kwa umakini kwa sababu kuanzia sasa mapambano dhidi ya ugaidi ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku,'' alisema Rais kabore.
Rais Kabore amesema kwa mara ya kwanza Burkina Faso imekuwa mhanga wa mashambulizi ya kishenzi ya kigaidi yenye lengo la kuiyumbisha nchi hiyo. Rais huyo aliyechaguliwa mwezi Novemba kuiongoza nchi hiyo katika uchaguzi wa kwanza huru katika kipindi cha miaka 50 alichukua madaraka wiki chache kabla ya kufanyika mashambulizi hayo.
Maafisa wamesema karibu ya watu 70 wamejeruhiwa vibaya katika mashambulizi hayo yaliyotokea Ijumaa jioni kwenye mgahawa wa Cappuccino na hoteli ya karibu ya Splendid. Kiasi ya raia 14 wa kigeni wanaaminika kuwa miongoni mwa watu waliouawa. Imeripotiwa kuwa raia wawili wa Uswisi, Mholanzi mmoja, Mmarekani mmoja na raia sita wa Canada wameuawa na taarifa hizo zimethibitishwa na wizara za mambo ya nje za nchi hizo.
Ufaransa na Italia pia zina wahanga
Vyombo vya habari vya Ufaransa vimeripoti kuwa raia wawili wa Ufaransa na Mreno mmoja anayeishi Ufaransa, wameuawa. Ofisi ya mambo ya kigeni ya Italia imesema mtoto wa mmiliki wa mgahawa huo raia wa Italia, mwenye umri wa miaka 9 ameuawa pia kwenye mashambulizi hayo.
Wanamgambo wa tawi la Al-Qaeda kwenye eneo la Maghreb-AQIM, wamedai kuhusika na mashambulizi hayo ambayo yaliendelea usiku kucha hadi Jumamosi, huku taarifa za hapa na pale zikisema milio ya risasi na miripuko ilikuwa ikisikika.
Serikali ya Burkina Faso imesema inaendelea na zoezi la kuwatambua wahanga wa mashambulizi hayo, ikisema kazi hiyo inafanyika taratibu kwa sababu ya idadi kubwa ya watu waliouawa.
Wakati huo huo, Burkina Faso na Mali zimekubaliana kufanya kazi kwa pamoja katika kupambana na kitisho kinachoongezeka cha wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu kwenye eneo la Afrika Magharibi.
Nchi hizo zimekubaliana kupeana taarifa za kijasusi na kufanya doria ya pamoja ya usalama kutokana na mashambulizi mawili yaliyopangwa vizuri na kusababisha mauaji katika eneo hilo. Mawaziri Wakuu wa nchi hizo mbili walikutana jana, siku ya pili baada ya kufanyika mashambulizi hayo mjini Ouagadougou.
Waziri Mkuu wa Burkina Faso, Paul Kaba Thieba na mwenzake wa Mali, Modibo Keita wamesema nchi hizo mbili zina utashi wa kisiasa katika kuunganisha nguvu na juhudi za kupambana na ugaidi. Matamshi hayo waliyatoa baada ya kuzuru kwenye hoteli ya Splendid iliyoshambuliwa.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,APE,DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman