1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 160 wauwawa BurkinaFaso

7 Juni 2021

Burkina Faso iko kwenye siku ya tatu za maombolezo ya kitaifa baada ya umwagikaji mkubwa wa damu uliofanywa na kundi la itikadi kali katika kijiji kimoja

Symbolbild Burkina Faso  Mehr als 138 Tote bei Anschlag
Picha: Issouf Sanogo/AFP

BurkinaFaso iko katika maombolezo ya kitaifa ya siku tatu kuanzia siku ya Jumamosi hadi hii leo kufuatia kuuwawa kiasi watu 160, wakiwemo takriban watoto 20, kwenye mashambulizi mabaya kabisa yaliyofanywa na kundi la itikadi kali. Mauaji hayo yametokea katika eneo la mpaka baina ya nchi hiyo na Mali na Niger.

Mauaji hayo yaliyoripotiwa kwa mara ya kwanza siku ya Jumamosi ndiyo makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Burkina Faso tangu mwaka 2015 na yalitokea katika kijiji kimoja kwenye eneo lenye hali tete ya usalama la kaskazini mwa nchi hiyo.

Mauaji hayo kimsingi yalifanyika usiku wa kuamkia Jumamosi baada ya watu wengine 14 kuuwawa siku ya Ijumaa katika kijiji cha Tadaryat kwenye eneo hilo hilo la kaskazini ambako waasi wenye kufungamana na mtandao wa Al Qaida na wale wanaojiita Dola la Kiislamu kufanya mashambulizi ya kuwalenga raia.
 

Taarifa za mwanzo zilizotolewa na vyanzo ndani ya eneo hilo zilisema kwamba waliouwawa ni watu 138 wakati serikali ikisema ni watu 132 waliouwawa na kiasi 40 waliojeruhiwa.

Katika kijiji cha Solhan kwenye eneo la karibu na mipaka ya Mali na Niger, wenyeji wamearifu kwamba jumla ya maiti 160 zimekutwa kwenye makaburi matatu tofauti. Chanzo kimoja kikaeleza kwamba wenyeji wa kijiji hicho wenyewe waliamua kufukua makaburi hayo na kuitoa miili na kuanza kuizika baada ya kuisafirisha.

Afisa mmoja amesema hali katika eneo la Solhan bado ni tete, licha ya kutangazwa kuwepo operesheni ya kijeshi. Imeelezwa na afisa mmoja  wa eneo hilo kwamba wakaazi wa kijiji hicho wanakimbia kuelekea miji ya karibu ya Sebba na Dori. Ameongeza kusimulia kwamba watu wengi wamepoteza kila kitu baada ya nyumba zao na mali kuteketezwa.

Picha: Str/AFP

Rais Roch Marc Christian Kabore siku ya Jumamosi alilaani mauaji ya Solhan akiyaita kuwa ukatili mkubwa na usioelezeka. Rais huyo aliwaomba Waburkinafaso kuendelea kushikamana na kusimama imara dhidi ya makundi ya itikadi kali. Siku tatu za maombolezo ya kitaifa zilizotangazwa kuanza Jumamosi zinamalizika leo Jumatatu.

Serikali ya Burkinafaso imewaita magaidi wale waliofanya mashambulizi hayo ya mauaji ya watu wa rika mbali mbali na kuchoma moto makaazi ya watu na soko kubwa la eneo hilo.

Picha: UNTV /AP/picture alliance

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres, Stephane Dujarric, amesema mauaji hayo ya watu wengi ni ya kushtuwa ambapo katibu mkuu Gutteres amelaani tukio hilo na kusisitiza haja ya dharura ya Jumuiya ya kimataifa  kuongeza msaada kwa nchi zinazopambana dhidi ya makundi ya itikadi kali katika eneo hilo. Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeongeza kusema kwamba inaiunga mkono kikamilifu  serikali ya Burkina Faso.

Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean Yves Le Drian ametangaza kufanya ziara wiki hii nchini Burkina Faso baada ya kuzungumza kwa simu na Rais Kabore.

Baada ya sala ya Jumapili, kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis naye aliwaombea wahanga wa umwagikaji huo wa damu nchini Burkina Faso.

Wakati huo huo, tukio jingine lililoripotiwa jana kuhusu harakati za itikadi kali ni kujiuwa kwa kiongozi wa kundi la itikadi kali la Boko Haram la Nigeria, Abubakar Shekau, ambaye imeelezwa alijitowa uhai katika mapigano dhidi ya wapiganaji wa kundi jingine la itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu la Afrika Magharibi - ISWAP.

Tukio hilo limejulikana kufuatia rekodi ya sauti iliyorushwa na shirika la habari la AFP iliyoipata kutoka chanzo cha  kundi hilo. Mkanda huo wa sauti umekuja wiki mbili baada ya kuibuka ripoti zikisema kwamba Shekau alishakufa.

Kifo cha kiongozi huyo wa Boko Haram kinaanzisha mwanzo wa mabadiliko katika uasi wa miaka 12 wa kundi hilo la itikadi kali ambao umeshaua zaidi ya watu 40,000 na kiasi milioni mbili ya wengine kuachwa bila makaazi huko kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW