1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ilwaidhulumu watu kabla ya kura ya maoni Burundi.

Shisia Wasilwa
18 Mei 2018

Vyombo vya usalama pamoja na tawi la vijana la chama tawala nchini Burundi CNDD-FDD viliua, kunajisi, kuwateka watu nyara, kudhulumu na kuwatisha wapinzani miezi michache kabla ya kura ya maoni iliyofanyika Alhamisi.

Burundi Wahlen
Picha: Getty Images/AFP

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema kwenye ripoti yake iliyotolewa Ijumaa tarehe 18.05.2018. 

Ripoti yakosoa serikali

Ripoti hiyo yenye kurasa 32 yenye mada ''Tutakupiga ili kukurekebisha; Unyanyasaji kabla ya kura ya maoni Burundi'' inaelezea mateso yaliyofanywa na vyombo vya usalama, shirika la huduma za upelelezi na wanachama wa tawi la vijana wa chama tawala, Imbonerakure pamoja na makundi mengine yaliyo karibu na chama tawala, mwaka mmoja na nusu kabla ya kura ya maoni kufanyika.

Waathiriwa wengi walilengwa kwa kukataa kujiandikisha kupiga kura na kuchangia fedha za kugharamia kura hiyo ya maoni.

"Kura ya maoni nchini Burundi ilifanyika katika mazingira ya wasiwasi, dhuluma na shinikizo," mazingira yanayotajwa na Ida Sawyer, mkurugenzi wa Shirika hilo katika taifa la Jamhuri ya Afrika ya Kati, "yasiyofaa kwa uchaguzi huru. 

Kura ya maoni ilifanyika Alhamisi, BurundiPicha: DW/A. Niragira

Anaongeza kusema, "kundi la Imbonerakure pamoja maafisa wa serikali walifahamu kuwa hapatakuwa na adhabu dhidi ya vitendo vyao vya ghasia ili kumruhusu Rais Pierre Nkurunziza kuendelea kubakia madarakani."

Iwapo upande wa 'Ndio' utashinda, mageuzi ya katiba yatamruhusu Rais Nkurunziza kusalia madarakani hadi mwaka 2034. Matokeo ya kura hiyo ya maoni yanatarajiwa kutangazwa muda wowote kuanzia leo.

Shirika la Human Rights Watch liliwahoji zaidi ya watu 100 kati ya mwezi Februari na Mei wakiwemo wakimbizi walioko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Uganda na wanachama wa zamani wa Imbonerakure. Wengi walisema hawakuwa na namna, isipokuwa kuikimbia nchi hiyo.

Mazingira hayakuwa huru kwa kura ya maoni

Lewis Mudge ni pia alichangia kuandaa ripoti hiyo, anasema, "tunatoa wito wa kwa viongozi wa kanda na Afrika Mashariki, kujitokeza na kushinikiza kukabiliwa kwa visa hivyo na kwa kiwango kingine watu wawajibike kwa ghasia walizotekeleza kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita."

Vyombo vya usalama vyashutumiwa kwa mauaji na vitishoPicha: picture-alliance/AP Photo

Ripoti hiyo imevitaja visa 15 vya mauaji, sita vya ubakaji vilivyotekelezwa kama adhabu dhidi ya walioonekana kuwa kinyume cha chama cha CNDD-FDD, vinane vya utekaji nyara miongoni mwa dhulma nyingine nyingi.  Alipokuwa akitangaza kura hiyo ya maoni tarehe 12 mwezi wa Desemba mwaka 2017, Nkurunziza aliwaonya wale waliokuwa na nia ya kuhujumu mpango huo wa kufanyia mageuzi katiba kwa maneno au vitendo. 

Ripoti hiyo inaeleza kuwa maafisa wake waliwahoji waliokuwa wanachama watano wa kundi la Imbonerakure kuhusu jinsi walivyokuwa wakitekeleza vitendo vyao tangu mwaka 2015. Mmoja wa waasi wa kundi hilo aliyekuwa mwanachama wa FNL alisema kuwa alijiunga na kundi hilo bila ya kupenda kisha akatoroka kwa sababu alikataa kuua. Anaongeza kusema kuwa alitakiwa kuthibitisha kuwa alikuwa mwanachama kamili kwa kuua.

Mwezi Oktoba mwaka 2017, majaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC, waliagiza uchunguzi ufanywe kuhusu uhalifu uliotekelezwa nchini Burundi kuanzi mwezi Aprili mwaka 2015. Siku mbili baadaye Burundi ikawa nchi ya kwanza kujiondoa kwenye mahakama hiyo.   

Mwandishi: Shisia Wasilwa/Human Rights Watch Report

Mhariri: Grace Patricia Kabogo