1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBurundi

Burundi: Miaka 30 tangu kuuawa Rais Ndadaye

Bakari Ubena | Daniel Gakuba
21 Oktoba 2023

Oktoba 21, 2023, Burundi inaadhimisha kumbukumbu ya miaka 30 tangu kuuawa kwa Melchior Ndadaye, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia katika taifa hilo.

Bildergalerie 50-jähriges Jubiläum der Afrikanischen Union AU
Rais Melchior Ndadaye aliyeuawa Oktoba 21,1993 baada ya kuchaguliwa kidemokrasia na kuitawala Burundi kwa muda wa siku 100 tu.Picha: DABROWSKI/AFP/Getty Images

Mauaji hayo ni alama muhimu katika siasa za Burundi, kwa sababu yaliitumbukiza nchi katika ghasia mbaya za kikabila, na kuyazika kwa muongo mzima matumaini ya utawala wa kidemokrasia.

Kama ilivyo kwa jirani yake Rwanda, Burundi pia inazo jamii za Wahutu waalio wengi na Watutsi walio wachache, na ugomvi wa madaraka baina ya jamii hizo umesababisha kuuawa kwa mamia ya maelfu ya raia wasio na hatia.

Melchior Ndadaye aliuawa  siku 100 tu baada ya kuapishwa kuingoza Burundi na kuwa rais wa kwanza kutoka jamii ya Wahutu nchini humo. Mauaji hayo ya kikatili yaliitumbukiza Burundi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya miaka 10 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 300,000 kuanzia mwaka 1993 hadi 2006.

Alipochaguliwa kwa karibu asilimia 65 ya kura katika uchaguzi wa tarehe 1 Juni mwaka 1993, uliosifiwa na waangalizi kuwa huru na wa haki, wachambuzi wa siasa za Burundi waliona matumaini kwa mustakabali wa nchi hiyo ndogo ya Ukanda wa Maziwa Makuu ya Afrika ambayo zamani ilikuwa koloni la Ubelgiji.

Hayati Meja Pierre Buyoya Aliyekuwa Rais wa Burundi na ambaye Mahakama Kuu ya Burundi ilimkuta na hatia ya mauaji ya Rais Ndadaye na kumhuku kifungo cha maisha jela.Picha: Alexander Joe/AFP/EPA/picture-alliance

Matumaini hayo yalikuwa na msingi, kwa sababu kiongozi wa wakati huo, Meja Pierre Buyoya aliyeingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1987, alikubali kushindwa na kukabidhi madaraka kwa njia ya amani.

Soma pia: Burundi: Buyoya apewa kifungo cha maisha kwa mauaji ya Ndadaye

Katika hotuba yake kwenye sherehe ya kumuapisha tarehe 10 Julai, Rais Melchior Ndadaye alikuwa amesema amani kwa raia wote wa Burundi lingekuwa suala lenye kipaumbele katika utawala wake.

''Hakika inadhihirika wazi kuwa Warundi mnahitaji amani. Amani katika nchi yenu, amani katika wilaya zenu, amani katika mioyo yenu, amani katika familia zenu. Amani hiyo tunayoihitaji sote, tutaipambania kwa nguvu zote,'' alisema.

Kifo cha Ndadaye chafuatiwa na umwagaji damu 

Lakini ndoto njema ya amani kwa Burundi iligeuka jinamizi usiku wa Oktoba 21, 1993, wanajeshi walipoyavamia makaazi ya rais, wakamfunga Rais Ndadaye na kumpeleka katika kambi yao ambako walimuuwa kikatili na kumzika katika hali ya kudhalilisha.

Taarifa za kuuawa kwake zilisambaa kama moto wa kiangazi miongoni mwa wafuasi wake katika maeneo ya vijijini, wengi wao wakiwa Wahutu, ambao walijawa na ghadhabu na kuwageukia majirani zao wa jamii ya Watutsi na kuwauwa kinyama kwa kuwakatakata kwa mapanga na silaha nyingine za kijadi, kama kisasi kwa jeshi lililomuuwa kiongozi wao waliyemchagua.

Mzunguko wa ghasia na umwagaji damu uliendelea pale jeshi lililokosa nidhamu lilipojitosa katika vurugu hizo, na kutumia silaha za moto kuwalenga raia wa Kihutu.

Sylvestre Ntibantunganya aliyeongoza serikali ya mpito ya Burundi kuanzia Aprili 1994 hadi Julai 1996.Picha: PASCAL GUYOT/AFP via Getty Images

Sylvestre Ntibantunganya aliyeongoza serikali ya mpito ya Burundi kuanzia Aprili 1994 hadi Julai 1996, ameiambia DW kuwa kuuawa kwa Ndadaye kuliipokonya Burundi fursa ya amani na ustawi.

''Ninavyojua mimi,  Melchior Ndadaye  alikuwa na dhamira ya kupambana na umasikini uliokuwa umekithiri Burundi na alikuwa na mipango thabiti ili kulifanikisha hilo, lakini pia kuwasaidia Warundi waweze kuishi pamoja kwa amani,'' alisema Ntibantunganya, na kuongeza kuwa  kuuawa kwa Ndadayei ''kulichochea chuki miongoni mwa raia, ambayo matokeo yake ni vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 10.''

Uchunguzi wa mwaka 2002 uliofanywa na serikali ya Burundi pamoja na Fuko la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Idadi ya Watu, UNFPA, ulionyesha kuwa watu 116,059 waliuawa katika ghasia hizo za mwaka 1993.

Leo hii kila upande, Wahutu na Watutsi, unadai jamii yake ilifanyiwa mauaji ya kimbari, lakini hakuna mahakama yoyote ya kimataifa iliyoyaunga mkono madai hayo.

Uasi wa Kihutu na makubaliano ya Arusha

Baada ya kuuawa kwa Melchior Ndadaye, makundi kadhaa ya Kihutu yalianzisha vita vya msituni dhidi ya jeshi la serikali lililodhibitiwa kikamilifu na Watutsi, na uasi huo ulihitimishwa na uchaguzi wa Agosti 2015 uliofikiwa baada ya upatanishi wa viongozi wa kikanda, Afrika Kusini na Umoja wa Mataifa.

Upatanishi huo ulifanikisha makubaliano ya Arusha yaliyosainiwa Agosti 2000, ambayo yalichora ramani ya uongozi wa baadaye, na uchaguzi wa baada ya kipindi cha mpito. Chama kikuu cha Wahutu,  CNDD-FDD  (Conseil national pour la défense de la démocratie – Forces de défense de la démocratie) kilishinda uchaguzi huo, na kiongozi wake, Pierre Nkurunziza akatangazwa rais.

Aliyekuwa Rais wa Burundi hayati Pierre Nkurunziza (kushoto) akiwa na Aliyekuwa rais wa mpito wa Burundi Domitien Ndayizeye wakitia saini makubaliano ya amani Novemba 16, 2003Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Mnamo muhula wake wa kwanza wa miaka mitano Burundi ilikuwa na utulivu kiasi, chini ya katiba ambayo ilihakikisha makundi yote ya kijamii yanawakilishwa katika taasisi za kisiasa na za kiusalama, katika wizani wa asilimia 60 kwa Wahutu na asilimia 40 kwa Watutsi.

Soma pia: Burundi yawakamata maafisa wa kijeshi kwa mauaji ya Ndadaye mwaka 1993

Ahueni hiyo ilisambaratika mwaka 2015, baada ya Nkurunziza kugombea muhula wa tatu, hatua ambayo ilipingwa sio tu na vyama vya upinzani na mashirika ya kiraia, bali pia na baadhi ya maafisa waandamizi ndani ya chama chake na jeshini, waliosisitiza kuwa muhula huo ulikuwa kinyume cha katiba. Kwa mara nyingine Burundi ilijikuta katika mivutano iliyohusisha maandamano yenye vurugu, yaliyoishia katika jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililoshindwa la 13 Mei. Takribani Warundi 39,000 walikimbilia nchi za nje, na wengi wao wanaendelea kuishi katika mataifa jirani.

Tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu

Rais wa sasa (2023) wa Burundi Evariste NdayishimiyePicha: Bujumbura Amida Issa/DW

Tangu kuingia madarakani kwa rais wa sasa, Evariste Ndayishimiye mwaka 2020, Burundi inashuhudia hali ya utulivu, ingawa mashirika ya kutetea haki za binadamu yanaendelea kuandamwa, huku upinzani ukikandamizwa. Ripoti ya Human Rights Watch ya mwaka 2022 inatambua kuwa hatua fulani imepigwa katika kuweka mageuzi yanayolenga kuboresha haki za binadamu, na kuongeza lakini kuwa mageuzi hayo ''ni yenye utata, na hayaonyeshi dhamira ya kushughulikia mizizi ya uhalifu uliofanyika tangu mwaka 2015.''

Katika mazungumzo na DW, rais wa zamani wa Burundi Sylvestre Ntibantunganya amesema masaibu iliyoyapitia nchi hiyo katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, yameacha mafunzo mengi kwa raia wake.

''Funzo la kwanza ni kuwa Warundi wametambua sasa kuwa njia halali pekee ya kuingia madarakani ni kupitia sanduku la kura,'' amesema Ntibantunganya, na kuongeza kuwa taratibu ''sera ya vyama vingi vya siasa inaanza kuzoeleka.''

Funzo muhimu zaidi hata hivyo kulingana na maoni ya mwanasiasa huyo mkongwe, ni kuwa  ''Warundi wamefahamu kuwa chaguo bora la kusuluhisha tofauti zao pindi zinapojitokeza ni kwenda kwenye meza ya mazungumzo'' badala ya kuchukua silaha na kuanza kuuwana wenyewe kwa wenyewe.