1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yaanzisha msako dhidi ya waziri mkuu wa zamani

Admin.WagnerD19 Aprili 2023

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Burundi, Martin Nitereste amekiri kuwa polisi iliendesha msako nyumbani kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Alain Guillaume Bunyoni kufuatia waranti uliotolewa na Mahakama Kuu ya Sheria.

Burundi Alain-Guillaume Bunyoni, Minister für Sicherheit
Picha: Getty Images/AFP

Hata hivyo, Bunyoni hakukutwa nyumbani na hajulikani aliko. Msako huo umefanyika wakati ambapo mkurugenzi anayehusika na upelelezi wa nje Museremu Innocent Alfred akifutwa kazi. Aidha, kamanda wa kikosi cha polisi cha kutuliza ghasia Desire Uwamahoro amewekwa kizuizini kwa tuhumu za kutoa taarifa kwa Bunyoni. 

Katika mkutano na waandishi habari Waziri Nitereste amesema mahakama hiyo ilikuwa na taarifa ambapo ilitakiwa kupata uhakika wa taarifa hizo kutoka kwa muhusika ambaye Bunyoni. Amesema kuwa mahakama hiyo iliamuru kufanyika kwa msako nyumbani kwa Bunyoni, lakini hawafanikiwa kumpata.

Bunyoni anasakwa kuhusiana na uhaba wa fedha za kigeniPicha: Antéditeste Niragira/DW

''Ndiyo msako ulifanyika nyumbani kwake, lakini ripoti ya msako huo bado hayijatolewa. Na hata sababu za kumsaka  bado sijafahamishwa kwani hawakufanikuwa kumpata. Hivyo tunasubiri endapo atapatikana tutapewa taarifa zaidi.''

Hayo yamejiri wakati mkurugenzi anayehusika na upelelezi wa nje Museremu Innocent Alfred akifutwa kazi. Waziri wa mambo ya ndani amesema uamuzi huo umechukuliwa sabamba na kusakwa Bunyoni, lakini ni matukio mawili yasiyokuwa na mafungamano yoyote na kwamba tayari ameteuliwa afisa mwingine kuchukua nafasi hiyo.

Kuhusu kutiwa kizuwizini afisa wa ngazi ya juu wa Polisi, Kanali Desire Uwamahoro ambaye ni kamanda wa kikosi cha polisi cha kutuliza ghasia, Waziri Nitereste amesema uchunguzi juu yake bado unaendelea.

''Uwamahoro nilisikia ya kuwa amekuwa akihojiwa wakati uchunguzi ukiendeshwa na mahakama kuu ya sheria. Kama mnavyojuwa sio mimi ninayeongoza mahakama hiyo, na mahakama haiwezi kunipa ripoti papo hapo kabla ya kukamilisha uchunguzi wake.''

Imeelezwa kuwa kiini cha msako huo nyumbani kwa Bunyoni ni uhaba wa pesa za kigeni, kwani amekuwa akimiliki pesa nyingi za kigeni kinyume cha sheria, ambazo zimekuwa zikitumika kinyume cha sheria.

Tangu alipoondolewa kwenye wadhifa wake mwezi Septemba mwaka uliopita kwa tuhuma za kutomtii Rais Evariste Ndayishimiye, kulikuwepo na taarifa za uwezekano wa Bunyoni kukamatwa na kufikishwa mahakamani. Amida Issa, DW Bujumbura.