1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yahimizwa iahirishe uchaguzi

31 Mei 2015

Hayo yamejitokeza leo (31.05.2015) baada ya mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu mzozo unaoikabili Burundi uliofanyika jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.

Burundi Krisengipfel
Picha: DW/H. Bihoga

Uchaguzi nchini Burundi unatakiwa kuahirishwa kwa angalau mwezi mmoja na nusu na machafuko yote yakome. Hayo yamesemwa na viongozi wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya mkutano wa kilele kuhusu mzozo unaoikabili Burundi uliofanyika jijini Dar es Salaam hivi leo.

Mwenyeji wa mkutano huo rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete amesema, "Tumekamilisha hivi punde mkutano wetu wa pili kuhusu hali nchini Burundi. Tunajaribu kutafuta njia ya kuwasaidia raia wa Burundi wasuluhishe mzozo wao kwa amani na usalama katika mazingira ya sasa."

"Mkutano ukiwa na wasiwasi na mkwamo wa kisiasa nchini Burundi, unaitisha kucheleweshwa kwa uchaguzi kwa muda usiopungua mwezi mmoja na nusu," imesema taarifa ya pamoja iliyosomwa na katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Richard Sezibera, baada ya mkutano huo wa viongozi kukamilika.

Taarifa hiyo imezitaka pande zote zinazohusika katika mgogoro wa kisiasa wa Burundi zikomeshe machafuko na makundi yote ya vijana yaliyojihami silaha yapokonywe silaha.

Mzozo wa Burundi ulizuka baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumteua rais wa sasa Pierre Nkurunziza kama mgombea wake katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi ujao, akigombea awamu ya tatu mfululizo ya miaka mitano. Upinzani na makundi ya kutetea haki za binaadamu yanasema hatua hiyo inakiuka katiba ya nchi pamoja na mkataba wa amani uliosainiwa mwaka 2006 uliovimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka 13.

Serikali ya Burundi imesisitiza uchaguzi wa bunge utafanyika kama ilivyopangwa hapo Juni 5 licha ya wiki kadhaa za machafuko ya umma katika barabara za mji mkuu Bujumbura na mikoa iliyo karibu, ambayo yamesababisha vifo vya watu 30. Uchaguzi wa rais umepangwa kufanyika Juni 26.

Rais Nkurunziza hakuhudhuria

Mkutano wa kilele uliofanyika jijini Dar es Salaam umeonekana kama fursa muhimu kuutanzua mzozo wa Burundi, huku mazungumzo kati ya upande wa rais Nkurunziza na kambi ya upinzani yakiwa yamekwama. Hata hivyo viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamesita kumwambia Nkurunziza aondoke madarakani, na badala yake wakahimiza utangamano urejee Burundi.

Rais wa Burundi Pierre NkurunzizaPicha: Getty Images/AFP/F.Guillot

Rais Nkurunziza hakuhudhuria mkutano huo lakini amewakilishwa na waziri wake wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa, Alain Aime Nyamitwe. Msemaji wake amesema kiongozi huyo ataendelea na kampeni yake ya kutaka achaguliwe tena kuiongoza Burundi, ambayo imesababisha machafuko na wimbi kubwa la wakimbizi kukimbilia mataifa jirani.

Ni wakati wa mkutano wa kwanza wa kilele kuhusu Burundi uliohudhuriwa na rais Nkurunziza mnamo Mei 13 mwaka huu ambapo jenerali wa ngazi ya juu wa Burundi alifanya jaribio la mapinduzi ambalo lilifeli kumng'oa madarakani kiongozi huyo, ambaye sasa anaonekana hataki tena kusafiri nje ya nchi hiyo.

Jumuiya ya Afrika Mashariki inazijumuisha Kenya, Rwanda, Tanzania, Burundi na Uganda. Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta wamehudhuria kikao hicho. Hata hivyo rais wa Rwanda, Paul Kagame, hakuhudhuria mkutano huo na badala yake amemtuma waziri wa Rwanda anayehusikana masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Valetine, Rwagweviza, kama muwakilishi. Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma pia amehudhuria mazungumzo hayo yaliyotanguliwa na kikao cha mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mwandishi:Josephat Charo/AFP/Reuters

Mhariri:Mohammed Dahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW