Burundi yajiandaa kwa uchaguzi wa bunge
1 Julai 2005Kwa mara ya kwanza tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipotipuka 1993, Burundi inatarajiwa kuwa na uchaguzi wa bunge wa kidemokrasi Jumatatu ijayo, huku chama cha waasi wa zamani CNDD-FDD kikitazamiwa kibuka na ushindi. Uchaguzi huo utafuatia ule wa madiwani uliofanyika mwezi uliopita.
Kampeni ya uchaguzi huo wa bunge inamalizika rasmi kesho Jumamosi tayari kwa uchaguzi Jumatatu, na ambao utafuatiwa baadae na ule war ais Agosti 19. Rais mpya atachaguliwa na kongamano la mabaraza mawili-bunge na baraza la Senate, ambalo litachaguliwa tarehe 29 ya mwezi huu na wajumbe wa mikoa. Tayari inaonekana CNDD-FDD litalidhibiti baraza hilo kutokana na ushindi wa 57 asili mia katika uchaguzi wa madiwani.
Wachambuzi wanasema hatua hiyo ni muhimu kabisa katika mlolongo wa taratibu za utekelezaji wa mkataba wa amani, uliosainiwa Arusha –Tanzania 2001 kwa lengo la kumaliza mgogoro ulioikumba nchi hiyo.
Tayari mwezi uliopita Mwenyekiti wa CNDD-FDD Pierre Nkurunziza, alitamka kwamba atakua mgombea Urais. Chama hicho ambacho kina wafuasi kutoka makabila yote mawili,huku wengi wakiwa Wahutu, kilianza mapigano 1993 dhidi ya jeshi la serikali lililokua likidhibitiwa na Watutsi walio wachache na mwishoni mwa 2003 kikakubali kusitisha mapigano na kujiunga na mwenenbdo wa amani. Chini ya makubaliano hayo jeshi jipya la taifa limeundwa miezi michache iliopita likiwa na 50 asili ya Wahutu na 50 asili mia watutsi.
Hata hivyo chama kingine cha waasi FNL, kimeendelea na mashambulio licha ya Kiongozi wake Agathon Rwasa kutangaza karibuni mjini Dar es salaam-tanzania kwamba kinakubali kusitisha mapigano. Hujuma za karibuni ni pamoja na zile za mkesha wa uchaguzi wa madiwani kwenye vitongoji vya mji mkuu-Bujumbura mwezi uliopita.
Hadi sasa kampeni ya uchaguzi wa bunge itakayomalizika kesho imefanyika katika hali ya usalama na utulivu.Pamoja na hayo Mnadhimu mkuu wa majeshi Jenerali Germain Niyoyankana alionya kwamba“FNL watakua na nia ya kuvuga uchaguzi, lakini tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha tunawadhibiti na uchaguzi unafanyika kwa usalama na utulivu.“
Kwa mujibu wa katiba mpya ya Burundi iliokubaliwa na umma Februari mwaka huu, bunge la taifa litakua na 60 asili mia ya wahutu ambao ni 85 ya wakaazi jumla na 40 ya watutsi walio 14 asili mia. Tangu uhuru kutoka Ubeligiji 1962 , watutsi ndiyo waliokua wakidhibiti hatamu za Uongozi na kusababisha mgogoro wa miaka mingi, mauaji na vita vya wenyewe kwa wenye. Leo, Burundi inaadhimisha miaka 43 ya uhuru huo.