1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBurundi

Burundi yakana madai ya kuuawa kwa mamia ya wanajeshi wake

16 Januari 2025

Burundi imesema wanajeshi wake waliotumwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kusimamia usalama wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Machafuko ya DR Congo
Sehemu ya kikosi cha Burundi kilichoko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kusaidia katika operesheni ya usalamaPicha: Alexis Huguet/AFP

Hayo yameelezwa na msemaji wa Jeshi la Burundi, Brigedia Jenerali Gaspard Baratuza, ambaye amekanusha vikali madai kwamba zaidi ya wanajeshi 200 wa Burundi wameuawa na waasi wa M23.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Brigedia Jenerali Gaspard Baratuza alieleza kuwa wanajeshi wa Burundi wanaendelea na jukumu lao la kuhakikisha amani na usalama mashariki mwa DRC. 

Amnesty International yamshutumu Rais Ndayishimiye kwa ukiukaji wa haki

Aliongeza kuwa wanajeshi hao wana mahusiano mazuri na raia wa maeneo hayo, hali inayodhihirika kwa raia kuwa na uhuru wa kuendesha shughuli zao za kawaida. Alisisitiza kuwa maeneo kama Uvira hadi Bukavu yamekuwa tulivu, na shughuli za usafiri na maisha zinaendelea hata nyakati za usiku. 

Hata hivyo, msemaji huyo alikanusha madai yanayosambazwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwamba waasi wa M23 wamewaua wanajeshi wa Burundi zaidi ya 200 katika eneo hilo. Brigedia Jenerali Baratuza alisema:

"Jeshi la Burundi linapinga vikali taarifa hizo za uongo zinazolenga kulichafua jeshi letu na kusababisha hofu miongoni mwa wananchi. Taarifa hizo ni njama za kuwavunja moyo wanajeshi wetu,"  amesema Jenerali Baratuza.

Hata hivyo, Baratuza alikiri kuwa wanajeshi wanaweza kupoteza maisha kwenye uwanja wa mapambano. Alisema kuwa jeshi lina taratibu maalum za kuwajulisha familia za wanajeshi waliopoteza maisha na kuhakikisha wanapewa heshima ya mazishi, na kuongeza. 

Tanzania na Burundi zawahamasisha wakimbizi kurejea kwao

Haimaanishi kuwa wanajeshi hawapotezi maisha. Wako kwenye uwanja wa mapambano, na kifo kinaweza kutokea popote pale, hata bafuni. Lakini kufa uwanjani ni kufa kwa heshima, kulingana na mikataba tuliyoisaini. Tunapofiwa na mwanajeshi, hatutangazi hadharani, lakini pia hatufichi. Familia zao hujulishwa rasmi na maiti zao huletwa kwa mazishi, iwe kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati au Somalia. 

Tamko hili la Brigedia Jenerali Baratuza limekuja wakati ambapo kumekuwa na madai kwamba waasi wa M23 wamewaua wanajeshi wa Burundi zaidi ya 200. 

Uwepo wa wanajeshi wa Burundi mashariki mwa DRC unatokana na makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya usalama kati ya viongozi wa nchi hizi mbili. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW