Burundi yapiga kura ya maoni kubadilisha katiba
17 Mei 2018Wananchi wa Burundi wamejitokeza leo kushiriki mchakato wa kupiga kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya katiba. Mabadiliko hayo ya katiba, yatakampa nafasi Rais Pierre Nkurunziza kuweza kutawala hadi 2034. Mchakato huo unafuatiliwa kwa karibu hasa na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu. Hatua hiyo imezua hofu ya ukandamizaji mkubwa wa kisiasa na migogoro ya kikabila katika taifa hilo la Maziwa Makuu.
Karibu watu nusu milioni wamekimbia tokea Nkurunziza kushinda muhula wa tatu wa urais katika uchaguzi uliokuwa na ghasia wa mwaka 2015.
Nkurunziza, mwalimu wa zamani wa riadha na aliyekuwa kiongozi wa vita vya msituni kutoka katika kabila la wengi la Hutu, amekuwa akiliongoza taifa hilo tokea mwaka 2005 vilipomalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya watu 300,000.
Sikiliza mahojiano ambayo Saumu Mwasimba alifanya na msemaji wa kundi la Muungano wa Vyama vya Upinzani-CINARED walioikimbia Burundi, Pancrase Chimpaye na kwanza anazungumzia mtazamo wa kundi hilo kuhusu mchakato unaoendelea Burundi.
Mwandishi: Saumu Mwasimba/Daniel Gakuba
Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman