1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali ya wapinzani Burundi yapigwa mnada bila wenyewe kuwepo

Daniel Gakuba
11 Novemba 2020

Wizara ya sheria ya Burundi imetoa tangazo kupitia redio na televisheni ya taifa, ikiwaalika wanunuzi katika mnada wa mali ya wapinzani inayoshikiliwa na mahakama ambao utaendelea hadi Jumamosi wiki hii mjini Bujumbura.

Burundi Präsident Evariste Ndayishimiye
Rais wa Burundi, Evariste NdayishimiyePicha: Tchandrou Nitaga/AFP

Mali hiyo inayouzwa mnadani ni ya wapinzani wa serikali wapatao 30, ambayo ilikamatwa mwezi Mei mwaka jana chini ya amri ya mahakama. Watu wote hao walipinga hatua ya rais wa zamani wa Burundi, hayati Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu mwaka 2015.

Miongoni mwao ni aliyekuwa makamu wa rais Bernard Busokoza, aliyekuwa msemaji wa chama tawala cha CNDD-FDD Onesme Nduwimana, mpinzani maarufu Alexis Sinduhije na mkurugenzi wa kituo cha kuwalea watoto yatima cha Maison Shalom, Marguerite Barankitse. Bi Barankitse amekosoa alichokiita, kumchanganya yeye na kituo anachokiongoza.

Marguerite Barankitse, mmoja wa wakosoaji ambao mali yao inapigwa mnadaPicha: DW

''Nimearifiwa kuwa wamekwenda katika mkoa wa Ruyigi mashariki mwa nchi, na kuchukua magari ambayo ni mali ya kituo cha Maison Shalom  na pia mali yangu binafsi'', amesema Bi Barankitse na kuongeza kuwa mali ya Maison Shalom ni mali ya watoto wa kituo hicho ambacho kimesajiliwa kisheria.

Vinara wa mapinduzi pia kupoteza mali yao

Wengine kwenye orodha ya watu ambao mali yao inauzwa katika mnada huo ni wanajeshi tisa waliohukumiwa kifungo cha maisha kwa hatia ya kuhusika katika jaribio la mapinduzi lililoshindwa la Mei 13, 2015, wakiwemo Jenerali Godefroid Niyombare, na Jenerali Cyrille Ndayirukiye, waziri wa zamani wa ulinzi, aliyekuwa miongoni mwa viongozi wa mapinduzi hayo. Wakili wake, Bernard Maingain anakosoa mnada huo.

''Utaratibu wa namna hii unalenga kuwafanya mafukara watu walioko jela, na kuvifanya vifungo vyao kuwa vibaya zaidi'', amelalamika wakili Maingain, na kueleza kuwa wakosoaji hao wa serikali wanapaswa kupewa haki ya kusubiri matokeo ya rufaa katika mahakama ya juu na mahakama ya haki za binadamu kabla ya mali zao kuchukuliwa.

Jaribio la mapinduzi la Mei 2020 dhidi ya rais wa zamani Pierre Nkurunziza liliitumbukiza Burundi katika mzozo mkubwaPicha: picture-alliance/AP Photo

Mnada kuendeshwa kwa siri

Kulingana na mwenyekiti wa shirika la kutetea uhuru wa asasi za kiraia nchini Burundi Vital Nshimirimana, mnada huu utaacha athari zisizoweza kutathminika. Anasema familia nyingi zitapokonywa kila kitu, na watoto ambao nyumba za familia zao zitauzwa, watajikuta wakiranda mitaani.

Chanzo kimoja ambacho hakikutaka kutajwa jina, kimeiambia DW kuwa waandishi wa habari ndani ya Burundi hawaruhusiwi kuripoti mchakato wa mnada huo. Juhudi za DW kupata kauli ya waziri wa sheria wa Burundi, Jeanine Nibizi, hazikuzaa matunda.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW