1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yarekodi visa vya kwanza vya mpox

26 Julai 2024

Waziri wa afya wa Burundi ametangaza kubainika kwa visa vya kwanza vya ugonjwa wa homa ya nyani, Mpox nchini humo, hali inayozusha hofu kwamba kirusi hicho kipya na kikali zaidi kimevuka mpaka.

Homa ya nyani
Burundi yarekodi visa vya kwanza vya mpoxPicha: Dado Ruvic/REUTERS

Mpox, zamani monkeypox, ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vinavyohamishwa kwa binadamu kutoka wanyama walioambukizwa na ambavyo vinaweza kuambukiza miongoni mwa wanadamu kupitia kugusana kimwili.

Mlipuko wa kimataifa miaka miwili iliyopita ulipelekea shirika la afya duniani, WHO, kuitangaza mpox kuwa janga la dharura la kiafya linalozusha wasiwasi kimataifa, ambayo ni tahadhari kubwa zaidi linaloweza kutoa.

Mamlaka ya Burundi iliarifiwa mnamo Julai 22 kuhusu "washukiwa" watatu katika hospitali mbili, moja katika wilaya ya wafanyakazi ya mji mkuu wa kiuchumi wa Bujumbura na mwingine nje kidogo ya jiji, taarifa ya wizara ya afya ilisema.

Shirika la Afya Ulimwenguni llimetahadharisha kwamba homa ya nyani bado ni kitisho cha kiafya

"Vipimo vya sampuli hizo tatu vilibaini kuwepo maambukizi ya Monkeypox," ilisema wizara hiyo, ikiongeza kuwa watu hao watatu "wanaendelea vyema, na orodha ya watu walioawasiliana nao tayari imeundwa na inafuatiliwa".

Mnamo Julai 11, WHO ilionya juu ya mlipuko mkubwa wa aina mpya ya virusi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambayo inapakana na Burundi. Mlipuko huo "hauonyeshi dalili ya kupungua," alionya mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Wakati huo, WHO iliripoti jumla ya visa 11,000, vikiwemo vifo 445, huku watoto wakiwa ndiyo walioathirika zaidi.

Chimbuko la Mpox

Mtoto wa miaka 6 Angelika Lifafu anaeugua ugonjwa wa nyani akionyesha namna mwili wake ulivyoathirika na ugonjwa huo. Picha: Arlette Bashizi /REUTERS

Rosamund Lewis, mtaalamu kiongozi wa WHO kuhusu mpox, alisema shirika la afya la Umoja wa Mataifa "lina wasiwasi sana" na kuonya kwamba virusi hivyo vinaweza "kuvuka mpaka kwa sababu mipaka kati ya mataifa hayo haina udhibiti wa kutosha. Mpox iligunduliwa kwa mara ya kwanza kwa binadamu mwaka 1970 nchini DRC.

Tangu wakati huo imekuwa ikijikita katika baadhi ya mataifa ya Afrika Magharibi na Kati, huku watu wakiipata kutoka kwa wanyama walioambukizwa, kama vile wakati wa kula nyama ya porini.

Kisha mnamo Mei 2022, maambukizo ya mpox yalienea kote ulimwenguni, yakiwaathiri zaidi wanaume wa jinsia mbili. Ongezeko hilo lilichochewa na aina mpya, iliyopewa jina la Clade II, ikichukua nafasi kutoka kwa aina ndogo ya Clade I.

Tahadhari ya kuenea kwa kirusi kipya cha homa ya nyani yatolewa Kongo

Lilikuwa ongezeko hilo katika visa lililosababisha WHO kutoa tahadhari ya dharura ya afya ya umma ya kimataifa mnamo Julai 2022, ambayo ilimalizika Mei 2023.

Lakini tangu Septemba iliyopita, aina mpya ya ugonjwa hatari zaidi wa Clade I imekuwa ikienea nchini DRC, huku mlipuko ukianza miongoni mwa wafanyabiashara ya ngono na kuathiri watu wasio wa jamii ya LGBTQ pia.

Uchunguzi ulibaini kuwa kilikuwa kirusi aina ya Clade I kilichojibadili, na kuzaa kirusi kipya cha Clade Ib. WHO inashauri watu waendelee kuwa macho juu ya virusi hivyo.

Chanjo ya ugonjwa wa Homa ya Nyani imepatikana

00:49

This browser does not support the video element.