1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yashusha kiwango cha kutoa fedha za kigeni

Amida Issa18 Septemba 2019

Benki kuu ya Burundi imeshusha kiwango cha fedha za kigeni kinachoweza kutolewa kwa siku, kutoka dola 3000 za kimarekani hadi dola 500 pekee

Symbolbild | Dollar Scheine
Picha: picture-alliance/dpa/S. Goya

Hatua hiyo imechukuliwa wakati hali ya uchumi wa nchi hiyo ya Afrika ya Kati ikizidi kuharibika. Gavana wa benki kuu wa Burundi  Ciza Jean, amesema  benki imefikia uamuzi huo kwa lengo la kuifanyia marekebisho sheria inayohusu matumizi ya fedha za kigeni nchini humo.

Kupitia marekebisho hayo kiwango cha fedha za kigeni ambacho mtu anaweza kukichukua kutoka  benki ni dola 500 za kimarekani, na hawezi kuzidisha dola 3000 kwa mwezi. Gavana Ciza  amesema hatua hiyo inakwenda sambamba na kuimarisha ukaguzi wa matumizi ya pesa za kigeni na kuoanisha mfumo wa Burundi na ule wa nchi nyingine za jumuia ya Afrika Mashariki.

Benki kuu ya Burundi imefanya marekebisho kwenye sheria juu ya matumizi ya pesa za kigeni iliyokuwepo tangu juni mwaka 2010. Lengo ni kuwianisha matumizi ya fedha hizo za kigeni na hali inayojiri kwa sasa na pia kuweka sawa  matumizi yake na mfumo unao fanya kazi katika nchi za Afrika mashariki.

Hata Raia wa kigeni wanaosafiri nchini Burundi au wanao ishi nchini humo walio na zaidi ya dola elf 10 wametakiwa kutoa ripoti kwenye taasisi husika la sivyo watakabiliwa na mkondo wa sheria. Aidha, Gavana huyo amesema hatua hizo zinayahusu pia maduka binafsi ya kubadilisha fedha ambayo yametakiwa kuheshimu kiwango kinacho pangwa na Benki kuu.

Maduka hayo yametakiwa kutoa risiti kwa kila operesheni ya kununua ama kuuza fedha za kigeni, na vile vile  wakati wowote ule kutoa nakala ya operesheni waliyoendesha ya kununua ama kuuza fedha za kigeni wanapotakiwa kufanya hivyo.

Habonimana Moussa, mwandishi wa habari za uchumi anasema hatua hizo zinadhihirisha kuzidi kuadimika fedha hizo za kigeni nchini humo, na hivyo kutatiza shughuli za kibiashara za bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi hususani mafuta ya petroli. Tangu mwaka 2015 nchi za magharibi ziliiwekea Burundi vikwazo na kusitisha kuipatia serikali ya nchi hiyo misaada ya kifedha.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW