1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bush aendelea na ziarani yake Ulaya yuko Italia

12 Juni 2008

-

Rais Bush atafuta uungaji mkono Italia kuhusu suala la Nuklia la IranPicha: AP

Kama ulivyosikia katika taarifa ya habari rais Goerge W Bush wa Marekani anafanya ziara ya siku mbili nchini Italia ambako atakutana na mshirika wake wa karibu waziri mkuu wa nchi hiyo Silvio Berlusconi.Ziara hiyo miongoni mwa masuala mengine ina lengo la kutafuta usaidizi katika vita vya Afghanstan pamoja na kutafuta uungaji mkono juu ya suala la Nukilia la Iran. Wakati huohuo wanaharakati wa kupinga vita na maelfu ya watu wamepanga maandamano makubwa katika barabara za mji mkuu wa Italia Roma kupinga ziara hiyo ya Bush.

Ziara hiyo ya rais wa Marekani imesababisha kuzuiwa safari za ndege za kibiashara zinazotuwa kwenye uwanja wa ndege wa mjini Roma huku mtreni ya mitaani pamoja na mabasi yanayoingia mji huo yakibadilishiwa njia za kupitia.

Maelfu ya polisi wamewekwa katika mji huo kuimarisha usalama na kudhibiti maandamano ya raia na wanaharakati wanaopinga vita. Jana maelfu ya watu waliandamana kuelekea ubalozi wa Marekani wakipiga kelele na kumtaja Bush ni Gaidi,Bush ni mbabe wa Vita na Italia ijitoe kwenye NATO. Waandamanaji walibeba mabango yaliyoandikwa wanajeshi wa nchi za magharibi waondoke Afghanstan na Lebanon.

Ziara ya siku mbili ya Bush itahusisha mkutano na waziri mkuu wa Italia Silvio Berlusconi ambaye alimuunga rais huyo katika vita vya Iraq kuanzia mwanzo ambapo alituma kikosi cha wanajeshi 3,000 nchini Iraq. Hata hivyo wanajeshi hao walirudi nyumbani na mara hii Berlusconi ameahidi hatowarudisha wanajeshi wake katika eneo hilo la vita.

Rais Bush anatafuta kuungwa mkono kwenye vita vya Afghanstan pamoja na msimamo wa kuiwekea ngumu Iran kuhusiana na mpango wake wa Nuklia ambao unadaiwa na nchi za Magharibi kuwa wenye lengo la kutengeneza silaha za maangamizi makubwa.

Kwa upande wake waziri mkuu wa Italia Silvio Berlusconi msimamo wake juu ya suala la Iran unakaribiana na ule wa Washington wakati mtangulizi wake kutoka chama cha mrengo wa kati kushoto Romano Prodi anapigia upatu kuweka mdahalo na Iran.Hata hivyo Berlusconi ambaye serikali yake iliyopita iliunga mkono uvamizi wa mwaka 2003 nchini Iraq anatazamiwa kuwabinya wanachama wenzake wa upande wa kihafidhina kuiongoza Italia kujiunga na kundi la nchi zenye nguvu katika kuongoza Diplomasia kwenye suala la Iran.

Aidha ziara ya Bush Italia ambako ni kituo chake cha tatu kwenye kile anachokiita ziara yake ya mwisho barani ulaya kama rais wa Marekani,atakutana pia na viongozi wa kibiashara,atafanya mazungumzo na rais wa nchi hiyo Giorgio Napolitano na baadae jioni watakuwa na mkutano na waziri mkuu Berlusconi pamoja na waandishi wa habari.Bush anatafuta njia ya kutia msukumo juhudi zake za kuitaka Ulaya kuimarisha vikwazo vya kimataifa vya kiuchumi dhidi ya Iran lakini juhudi hizo za Bush zinaonekana kama zitagonga mwamba nchini Italia ambayo ni mshirika mkubwa wa kibiashara barani ulaya wa Iran .

Bush pia anatarajiwa kuzungumza na Berlusconi kuhusu mpango wa amani wa Mashariki ya kati,hali ya mambo nchini Lebanon na juhudi za kuileta karibu na majirani zake wa Ulaya nchi changa ya Kosovo iliyopata uhuru hivi karibuni.

Kesho ijumaa atakutana na kiongozi wa kanisa katoliki duniani baba mtakatifu Benedict wa 16 mjini katika jumba la St Johns huko Vatican.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW