1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bush asema mkataba amani Mashariki ya Kati kupatikana katika kipindi cha mwaka mmoja

10 Januari 2008

RAMALLAH

Rais George W. Bush wa Marekani leo hii ametabiri kwamba mkataba wa amani Mashariki ya Kati utatiwa saini wakati atakapokuwa anaondoka madarakani katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja na hiyo kuwapatia Wapalestina taifa lao wenyewe waliokuwa wakilisubiri kwa muda mrefu.

Lakini katika ziara yake ya kwanza kwenye eneo la Wapalestina linalokaliwa kwa mabavu na Israel la Ukingo wa Magharibi Bush amesema pande zote mbili Israel na Wapalestina inabidi zifanye maamuzi magumu ili kufanikisha kupatikana kwa amani kutokana na kuendelea kuwepo kwa tafauti kubwa kama ilivyojionyesha kwenye mazungumzo ya amani yaliofufuliwa upya hivi karibuni.

Bush ambaye anatarajia kujipatia ushindi mkubwa wa sera za kigeni kabla ya kuondoka madarakani hapo mwezi wa Januari mwaka 2009 kufuatia kushindwa mara kadhaa kwa tawala zilizopita za Marekani kuleta amani amesema taifa la Palestina lazima lipakane na kuwa na ujirani mwema na Israel.

Katika ziara yake hiyo Bush pia alikwenda Bethlehem katika Ukingo wa Magharibi na hapo kesho anatazamiwa kuelekea Kuwait kituo chake cha pili cha ziara yake ya siku nane Mashariki ya Kati.