CAIRO: Mataifa ya Kiarabu yamuunga mkono Rais wa Palestina Mahmoud Abbas.
16 Juni 2007Mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa ya Kiarabu wametangaza wanamuunga mkono Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas hata baada ya chama cha Hamas kuteka Ukanda wa Gaza.
Kwenye kikao cha dharura cha Umoja wa Nchi za Kiarabu mjini Cairo, mawaziri hao pia wameamua kuandaa tume ya kuchunguza mzozo uliopo kati ya vyama vya Hamas na Fatah.
Hapo awali Katibu Mkuu wa Umoja wa nchi za Kiarabu, Amr Moussa, aliuzungumzia mzozo huo unaoendelea kati ya Hamas na Fatah.
Amr Moussa amesema:
"Ikiwa tunataka hali itengemae ni lazima pia tuzingatie kwamba watu wengi wanaishi katika hali ya kutawaliwa na majeshi ya kigeni maanake hali isiyoridhisha. Hilo ni lazima kulizingatia. Si suala la taifa na uchaguzi au serikali mbili zinazopishana. Wapalestina wenyewe wanapaswa kutambua hilo."
Rais Mahmoud Abbas amevunja serikali ya umoja wa kitaifa ya vyama hivyo viwili na akamteua mwanasiasa wa kujitegemea, Salam Fayyad aliyewahi kuwa waziri wa fedha, aongoze serikali ya mudai.
Chama cha Hamas kimesema hatua hiyo ya Mahmoud Abbas ni sawa na mapinduzi.
Shirika la msalaba mwekundu limesema vita kati ya wapiganaji wa vyama hivyo viwili vimesababisha watu kiasi mia moja na kumi na sita wauawe na wengine zaidi ya mia tano na hamsini wamejeruhiwa.