CAIRO : Waislamu walaani matamshi ya Papa
16 Septemba 2006Waislamu wamelaani matamshi juu ya Uislamu yaliotolewa na Papa Benedikt wa 16 na wengi wanataka kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani aombe radhi binafsi kuondoa dhana kwamba amejiunga na kampeni dhidi ya dini yao.
Umoja wa Nchi za Kiislam wa mataifa 57 OIC umesema nukuu zilizotamkwa na Papa ni sawa na kumchafulia jina Mtume Muhammad na ni kampeni ya kukashifu.Umoja huo unataraji kwamba kampeni hiyo haitokuwa utangulizi wa sera mpya ya Vatikani kwa Uislamu.
Katika hotuba yake wakati wa ziara yake nchini Ujerumani hapo Jumanne Papa Benedikt alimkariri Mfalme wa Karne ya 14 wa Byzantine aliesema kwamba Mtume Muhammad hakuiletea dunia kitu chochote kile isipokuwa uovu mathlan kwa uongozi wake wa kuitangaza kwa kutumia upanga dini aliyokuwa akiihubiri.
Bunge la Pakistan kwa kauli moja limelaani kauli hiyo ya Papa na imemtaka aintangue kauli hiyo.Chama tawala nchini Uturuki kimemlinganisha papa huyo na Hitler na Musssolini wakati waziri wa mambo ya nje wa Misri Ahmed Aboul Gheit amesema Papa Benedikt lazima ajieleze afafanuwe mwenyewe binafsi kile alichokuwa amekikusudia kusema.
Ingawa Papa mwenyewe hakudokeza iwapo alikuwa akikubaliana na matamshi hayo aliyoyakariri au la makao makuu ya Kanisa Katoliki Vatikani imesema Papa anaheshimu Uislamu na hakukusudia kuleta maudhi.Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema nia ya hotuba ya papa ilikuwa ni kuendeleza majadiliano miongoni mwa dini mbali mbali na kupinga kabisa utumiaji nguvu wowote ule kwa kutumia jina la dini.
Matamshi hayo ya Papa Benedikt kuhusu Uislamu na Jihad vita takatifu ambayo yamechemsha ulimwengu wa Kiislam wengi wanahofu yanaweza kuchochea maandamano ya ghasia kama yale yaliozuka kufuatia kuchorwa vikatuni vya kumdhihaki Mtume Muhammad SAW.