1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cameron abebeshwa lawama vita vya Libya

Zainab Aziz14 Septemba 2016

Bunge la Uingereza linasema waziri mkuu wa zamani, David Cameron, alikurupuka kuivamia Libya bila ya kuzingatia taarifa sahihi na hakuwa na mipango ya baada ya mashambulizi hayo, na hivyo kuiwacha imesambaratika.

Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, David Cameron, katika ziara yake mjini Tripoli, baada ya kuangushwa na kuuawa kwa Muammar Gaddafi.
Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, David Cameron, katika ziara yake mjini Tripoli, baada ya kuangushwa na kuuawa kwa Muammar Gaddafi.Picha: Getty Images/S. Rousseau - Pool

Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge, ambayo ilipewa jukumu la kuyatathmini kwa kina maamuzi ya Uingereza ya kujiingiza katika uvamizi nchini Libya ikishirikiana na Ufaransa mnamo mwaka 2011, inasema maamuzi ambayo serikali ya Cameron ilisema ni kuwalinda raia wa Uingereza kutokana na mashambulizi kutoka kwa aliyekuwa rais wa Libya, Muammar Gadaffi, hayakuwa sahihi.

Ripoti hiyo inasema kuwa serikali ya Uingereza ilishindwa kuthibitisha hatari iliyowakabili wananchi wake kutoka utawala wa Gadaffi na badala yake ilitoa maamuzi yake kulingana na maneno yaliyokuwa yakisemwa na kiongozi wa Libya.

Vile vile, ripoti hiyo inaelezea kushindwa kwa serikali ya Uingereza kutambua kwa haraka vielelezo vya Uislamu wenye itikadi kali kutoka kwenye vikundi vilivyokuwa vikimpinga Gadaffi.

Ripoti hiyo ya kamati ya mambo ya nje ya Uingereza imeongeza kusema kwamba mkakati wa Cameron ulijengwa na taarifa zisizo sahihi. Aidha ushahidi uliotumiwa kufikia maamuzi ya kushambulia Libya kwa mabomu haukueleweka vizuri.

Libya imesambaratishwa kila upande

Ni miaka mitano sasa tangu Gadaffi alipong'olewa madarakani na kuuwawa, na hali nchini humo imezidi kuchafuka makundi mawili hasimu yanazidi kupambana. Machafuko yote haya ni kwa sababu kila kundi linataka kuwa madarakani na pia linataka kudhibiti utajiri wa mafuta.

Kiongozi wa zamani wa Libya aliyepinduliwa na kuuawa kinyama, Muammar Gaddafi.Picha: imago/Anan Sesa

Crispin Blunt mwenyekiti wa kamati ya mambo ya nje ya Uingereza amesema ingekuwa bora kama serikali yake ingelijaribu kutumia njia zingine zilizokuwepo kwa ajili ya kuleta mafanikio nchini Libya kwa mfano mazungumzo ya kisiasa, kubadili utawala kwa njia mazungumzo au marekebisho katika sera za uongozi wa Libya ameeleza kuwa njia hizi zote zingeweza kuwalinda wananchi wa Libya kutokana na dhiki wanayoipata sasa.

Blunt pia ameongezea kusema kuwa Uingereza isingeingia kwenye gharama zozote wala haingepoteza chochote kama isingeamua kutumia nguvu za kijeshi kwa ajili ya kubadili utawala wa Libya.

Kamati hiyo imeripoti kuwa aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza alikataa kufika mbele yao kwa kudai hakuwa na muda kutokana na kazi nyingi lakini waziri mkuu wa ulinzi wa zamani Liam Fox waziri wa mambo ya nje wa zamani William Hague na pia waziri mkuu wa zamani Tonny Balir wote walifika mbele ya kamati hiyo kutoa ushahidi wao.

Azimio la baraza la usalama la umoja wa mataifa pamoja na nchi za kiarabu waliunga mkono na kuruhusu matumizi ya njia zote kwa ajili ya kuwalinda raia na hapo ndipo amri ya kusitisha mapigano na kuzuia kuruka angani ndege za majeshi ya serikali ya Gaddafi ilipoanza kufanya kazi.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW