Cameron, Merkel wajadili mageuzi ndani ya EU
13 Aprili 2013Merkel alimualika Cameron na mke wake Samantha, na watoto wao watatu katika kasri la wageni la serikali ya Ujerumani la Meseburg, lililoko umbali wa kilomita 70 kusini-magharibi mwa Berlin. Mazungumzo ya siri kati ya Merkel na Cameron yalipangwa kufanyika Ijumaa jioni na Jumamosi asubuhi. Msemaji wa Kansela Merkel, Steffen Seibert alisema kabla ya mazungumzo hayo siku ya Ijumaa, kuwa Uingereza ni mshirika muhimu sana kwa Ujerumani katika Umoja wa Ulaya.
Cameron ambaye chama chake cha kihafidhina kina kundi lenye nguvu linalopinga uanachama wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya, anafanya ziara kwa viongozi wa Ulaya, katika jitihada zake za kushinikiza mabadiliko ndani ya Umoja wa Ulaya, ikiwa ni pamoja na kuzipatia nchi wanachama haki ya kujitenga na baadhi ya sheria za umoja huo. Wiki hii alikatisha ziara fupi mjini Madrid Uhispania, na alikuwa akipanga upya mazungumzo na rais wa Ufaransa, Francois Hollande, baada ya kifo cha waziri mkuu wa zamani, Margaret Thatcher.
Cameron alikabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa Ujerumani na Ufaransa mwaka huu, alipotangaza mipango ya kujadili makubaliano mapya kwa Uingereza, na baadae kuendesha kura ya maoni kuhusu uanachama wa Uingereza kufikia mwaka 2017. Cameron alinukuliwa wiki hii akisema kuwa Ulaya itakuwa yenye mafanikio zaidi kama itakuwa na nguvu ya mabadiliko, kuliko udhaifu wa kutotaka mabadiliko. "Nadhani matokeo mazuri zaidi kwa Uingereza ni uanachama wetu wa Umoja wa Ulaya uliyofanyiwa mabadiliko," alisema waziri mkuu Cameron.
Ajenda nyingine za mkutano wao
Merkel na Cameron pia walipanga kujadili mpango wa nyuklia wa Iran, vita vya nchini Syria, na mkutano mkuu wa kilele wa Kundi la mataifa manane, utakaofanyika mwezi Juni katika Ireland ya Kaskazini, kwa mujibu wa msemaji wa Kansela Merkel. Ujerumani pia ilitrajiwa kuishinikiza Uingereza juu ya haja ya kuchukua hatua kushughulikia mataifa mbalimbali duniani, ambako baadhi ya kodi hutozwa kwa kiwango kidogo sana au hazitozwi kabisaa.
Kwa muda mrefu, wabunge wa Ujerumani wameonyeshwa kukatishwa kwao tamaa na uhusiano wa Uingereza wa kujitenga na Umoja wa Ulaya, ukiwemo uamuzi wa Cameron mwaka 2009, kukiondoa chama chake cha kihafidhina kutoka kundi la nadharia za mrengo wa kati, kuelekea kulia katika bunge la Ulaya, ambalo linajumuisha pia chama cha Kansela Merkel cha Christian Democratic Union, CDU.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape,dpae,rtre
Mhariri: Grace Patricia Kabogo