Cameroon na Ghana kuumana nusu fainali
2 Februari 2017Ghana ilionekana kujiweka haraka kuwa moja kati ya vigogo vya soka barani Afrika tangu kuanzishwa mashindano hayo, baada ya Misri kutawala soka la Afrika miaka miwili ya mwanzo tangu mashindano hayo yaliapoanzishwa mjini Addis Ababa mwaka 1957.
Ghana ilijiunga na mashindano hayo na kulinyakua kombe hilo kutoka kwa Misri mwaka 1963 na kulinyakua tena mwaka 1965, 1978 na 1982. Tangu wakati huo Ghana ilipotea kutoka katika kundi la vigogo vya soka barani Afrika na imefanikiwa tu kuingia katika fainali mara mbili katika miaka ya 2000, lakini haijaonja tamu ya kurejea nyumbani na taji hilo la bara la Afrika.
Cameroon nayo ikijivunia rekodi ya kulinyakua kombe hilo mara nne pia inawania mara hii kulipeleka taji hilo mjini Yaoude kwa mara ya tano. Cameroon ililinyakua kombe hilo mara ya kwanza mwaka 1984 na kisha mwaka 1988, 2000 na 2002.
Cameroon ilitokea kutoka kundi A katika mashindano ya mwaka huu ikifungwa katika mchezo wa kwanza na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwa bao 1-0 na kisha ikaishinda Guinea ya Ikweta kwa mabao 2-1, na kutoka sare na wenyeji wa mashindano hayo Gabon bila kufungana ikijitokeza kuingia duru ya robo fainali ikiwa namba mbili kutoka kundi hilo. Cameroon ilionesha makali yake pale ilipofanikiwa kuitoa kwa mikwaju ya penalti Senegal katika mchezo mkali na wa kuvutia wa robo fainali baada ya timu hizo kucheza kwa dakika 120 bila kufungana.
Safari ya Cameroon
Njia ya Cameroon kuelekea nusu fainali haionekani kuwa rahisi hivyo kwani ilipata ushindi mara moja tu wa wazi dhidi ya timu ndogo ya Guinea ya Ikweta, lakini pia kuishinda Senegal ambayo ilipigiwa upatu katika duru ya makundi kwamba huenda ndio itatawazwa mabingwa katika fainali hizi si jambo la kubezwa.
Inadhihirika wazi kwamba Cameroon mara hii ni imara zaidi katika ulinzi kuliko ushambuliaji , lakini timu yoyote inayoweza kuwasimamisha washambuliaji hatari wa Senegal , kina Sadio Mane , na Biram Diouf Mame inahitaji ukuta imara ambao utatumika hata leo kuwazuwia washambuliaji hatari wa Ghana , kina Andre Ayew na mdogo wake.
Ghana ambayo inaonekana kimahesabu kuwa bora zaidi ya Cameroon jioni ya leo itabidi kufanya kazi ya ziada kuuvunja ukuta wa Cameroon.
Ghana iliyokuwa katika kundi D , ilianza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wawakilishi kutoka Afrika mashariki Uganda, ikaifunga Mali pia kwa bao 1-0 na kufungwa bao 1-0 na Mafarao wa Misri lakini ikajihakikishia nafasi ya kucheza robo fainali ikiwa nayo katika nafasi ya pili nyuma ya Misri.
Lolote litakalotokea hii leo(02.02.2017) kati ya Cameroon na Ghana , Mafarao wa Misri watakuwa wanakodoa macho kuona ni mbinu gani watazitumia katika fainali dhidi ya yeyote kati ya timu hizo hapo tarehe 5 Jumapili.
Mwandishi: Sekione Kitojo /
Mhariri: Yusuf Saumu