1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cameroon:Watu 7 wauawa katika vuguvugu la kujitenga

Daniel Gakuba
2 Oktoba 2017

Watu wasiopungua 7 wameuawa katika Kaskazini Magharibi mwa Cameroon, sehemu inayotumia lugha ya Kiingereza, katika operesheni za vikosi vya usalama kuzima harakati za wanaotaka eneo hilo lijitangazie uhuru wake.

Kamerun - Proteste
Maelfu ya maafisa wa usalama walipelekwa sehemu ya vuguvugu la wanaotaka kujitengaPicha: Reuters/TV

 

Tangu mwezi Novemba watu wa sehemu hiyo ya Magharibi mwa Cameroon wamekuwa wakiandamana kupinga kile wanachokichukulia kuwa ubaguzi wanaofanyiwa na serikali inayozungumza lugha ya Kifaransa.

Hapo jana wanajeshi wengi wa serikali walipelekwa katika sehemu hiyo, hususan katika mji wa Buea Kusini Magharibi mwa mji mkuu zaidi katika eneo hilo, Bamenda. Duru za hospitali ya mji huo zimeeleza kuwa watu kadhaa walilazwa katika hospitali hiyo, mmoja wao akiwa na majeraha ya risasi. Chanzo kutoka hospitali hiyo kililieleza shirika la habari la AFP kuwa vikosi vya usalama vilitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji.

Mmoja wa viongozi wa chama cha upinzani cha Social Democratic Front, Joshua Osih, ambaye hata hivyo alijitenga na vuguvugu la kudai uhuru, amewashutumu polisi kufyatua risasi kiholela katika makundi ya waandamanaji.

Kisa ni kukatwa kwa intaneti

Watu wengine waliandamana kupinga makundi yanayotaka kujitengaPicha: Reuters/J. Kouam

Mzozo huu ulianza kushika kasi mwanzoni mwa mwaka huu wa 2017 kufuatia uamuzi wa serikali kuwakatia wakazi wa eneo hilo mtandao wa intaneti kwa muda wa miezi mitatu, na umeendelea kukua mnamo wiki za hivi karibuni, na kuwa shinikizo la kutaka eneo hilo linatumia Kiingereza lijitawale lenyewe.

''Sisi ni Waambazonia, hatutaki kitu kingine. Njia pekee ya kusuluhisha mzozo huu, ni serikali ya Paul Biya kutupa uhuru wetu'', amesema mwandamanaji mmoja kijana.

Kulingana na makadirio ya Shirika la Kimataifa linaloshughulikia mizozo, ICG, watu kati ya 30,000 na 80,000 waliandamana katika maeneo mengi ya sehemu ya Cameroon inayozungumza Kiingereza.

Kukoma kwa 'utumwa kwa Cameroon'

Mtu anayejitatambulisha kama rais wa Ambazonia, Sisiku Ayuk alifanya kitendo ambacho ni ishara tu, cha kutangaza uhuru wa eneo hilo kupitia mtandao wa kijamii, akisema, ''tumekoma kuwa watumwa wa Cameroon''. ''Leo tunatangaza rasmi mamlaka ya urithi wetu na eneo letu'' alisema Ayuk.

Kabla ya jana, serikali ya Cameroon ilikuwa imesimamisha safari kuelekea eneo hilo na kufuta mikutano yote, hayo yakiongeza juu ya sheria ya hali ya hatari iliyotangazwa katika sehemu hiyo na mkoa wa Kaskazini Magharibi.

Huduma ya intaneti imeondolewa tangu Ijumaa, licha ya ahadi ya serikali kwamba huduma hiyo isingeguswa katika mikoa inayozungumza Kiingereza.

Nchini Cameroon, raia milioni 22 hutumia lugha ya kifaransa, wachache waliobaki ambao ni kama asilimia 20 tu ya hao, ndio wanaotumia lugha ya Kiingereza.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe

Mhariri:Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW