CAPE TOWN Mark Thatcher afikishwa mahakamani Afrika Kusini.
18 Februari 2005Mfanyabiashara wa Uingereza, Mark Thatcher, amefikishwa mbele ya mahakama moja ya Afrika Kusini kujibu mashtaka ya kutaka kuipindua serikali ya Guinea ya Ikweta. Thatcher, mwanawe waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Margaret Thatcher, aliyajibu maswali yaliyowasilishwa na waongoza mashtaka wa serikali ya Guinea, wanaomtuhumu kwa kutaka kumpindua kiongozi wa taifa hilo, Teodoro Obian Nguema. Amekubali alivunja sheria ya mamluki ya Afrika Kusini kwa kusaidia kudhamini njama hiyo kwa kutoa helikopta, ambayo waongoza mashtaka wanadai ingetumiwa katika mapinduzi hayo. Lakini Thatcher amesema kwamba hakujua helikopta hiyo ingetumiwa katika njama hiyo, na akapinga kuhusika katika shughuli nyengine zinazohusiana na mpango huo. Mwezi Novemba mwaka jana, serikali ya Guinea ya Ikweta iliwahukumu watu 13, vifungo gerezani kwa kuhusika katika njama hiyo, wakiwemo raia 11 wa kigeni.