1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CARICOM: Waziri Mkuu wa Haiti kuandaa uchaguzi

29 Februari 2024

Viongozi wa nchi za kanda ya Karibea wamesema kwamba Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry amekubali kuandaa uchaguzi mkuu ifikapo katikati ya mwaka 2025.

Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry
Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry akihutubia ukatika mkutano wa hadhara mjini Port-au-Prince.Picha: Richard Pierrin/AFP

Haya yanajiri huku Umoja wa Mataifa ukitoa wito wa kuchangishwa dola milioni 674 kwa ajili ya misaada ya kiutu nchini humo.

Wanachama wa jumuiya ya kikanda ya kiuchumi - Caricom wametoa taarifa baada ya mkutano wa kilele wa siku nne huko Guyana wakisema Henry amekubali kwamba kuna haja ya kuandaa uchaguzi na kushirikiana na upinzani na makundi ya kijamii ili kufikia lengo hilo.

Taarifa hiyo ilisema kuwa wadau wote katika jamii ya Haiti, akiwemo Henry, watalazimika kushiriki makubaliano ili kuruhusu uchaguzi na kurejeshwa kwa demokrasia katika nchi hiyo maskini ambayo  haina viongozi waliochaguliwa kidemokrasia.

Wakuu wa jumuiya ya Caricom wameelezea wasiwasi wao mkubwa kuhusu kuendelea kuzorota hali ya usalama, kibinaadamu na kisiasa na kuendelea kucheleweshwa katika kuutatuwa mkwamo wa kisiasa ambao umezuia uwezekano wa kuandaliwa uchaguzi  huru na haki.

Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva ambaye pia alihudhuria mkutano huo ameitaka dunia kuchukua hatua za haraka katika kuishughulikia Haiti.

"Tunahitaji kuchukua hatua haraka ili kupunguza mateso ya watu walioathiriwa na janga hili,"

"Ni muhimu sana kwamba nchi eneo la Karibea, ujumbe wa Umoja wa Mataifa na viongozi wa Caricom kushiriki katika upatanishi kati ya wanasiasa wa Haiti." Aliongezea Lula da Silva.

Mustakabali wa demokrasia

Polisi wakizima moto, sehemu ya kizuizi kilichowekwa na waandamanaji Port-au-Prince, Haiti.Picha: AP

Wakuu wa Caricom wamesisitiza suala muhimu na la haraka la kuwepo ufafanuzi wazi wa njia ya kisiasa ambayo inapaswa kuwa shirikishi. Marekani Canada na Umoja wa Mataifa wataisaidia Haiti katika kuunda timu itakayofanya tathmini na kuisaidia kujiandaa kwa uchaguzi.

Msemaji wa ofisi ya Henry alikataa kutoa maoni kuhusiana na taarifa hiyo wakati waziri mkuu huyo akielekea Kenya baada ya kuondoka Guyana.

Soma pia: Serikali ya Kenya yaapa kupinga uamuzi wa mahakama dhidi ya kupeleka maafisa wa polisi nchini Haiti

Henry ameahidi mara kwa mara kufanya uchaguzi tangu kuapishwa kwake kama waziri mkuu baada ya mauaji ya Julai 2021 ya Rais Jovenel Moïse, lakini yeye na maafisa wengine wanasema ghasia zinazosababishwa na magenge ya wahalifu hazijawaruhusu kuendelea na ahadi hizo.

Katika mkutano na waandishi wa habari Waziri Mkuu wa Bahamas Philip Davis ameitaja hali ya Haiti kuwa ni "mbaya sana."

Mratibu wa masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti Ulrika Richardson amesema hali ya machafuko ni mbaya mno nchini humo.

"Watu wanakabiliwa na ukiukwaji wa kikatili na mbaya wa haki zao za kibinadamu. Wanafanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na ubakaji wa magenge, na tumeona ongezeko la asilimia 50 la ukiukaji wa ngono kati ya 2022 na 2023." Alisema Richardson.

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa dola milioni 674 kwa ajili ya misaada ya kiutu nchini Haiti ambako asilimia 45 ya idadi jumla ya watu nchini humo, hawana usalama wa chakula. Umoja wa Mataifa unasema, mwezi Januari pekee, zaidi ya watu 1,100 waliuwawa, kujeruhiwa au kutekwa nyara.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW