Catalonia huenda ikajitangazia uhuru wake
10 Oktoba 2017Wakati hotuba hiyo ikisubiriwa, kiongozi huyo ameendelea kupata shinikizo kutoka ndani na nje ya nchi akitakiwa kusitisha mpango huo. Hotuba hiyo anayotarajiwa kuitoa katika bungeni la jimbo la Catalonia, kiongozi wa jimbo hilo Carles Puigdemont, imeibua wasiwasi wa usalama katika Umoja wa Ulaya.
Viongozi wa kisiasa wamewatolea mwito Wacatalonia wanaotaka kujitenga kusitisha mpango wao huo na kuinusuru Uhispania na mgogoro mbaya zaidi katika miongo kadhaa iliyopita. Meya maarufu wa mji wa Barcelona Ada Colau amepinga azma ya Catalonia kujitangazia uhuru. "Oktoba mosi imefungua milango ya majadiliano. Imeiweka Catalonia katika ramani. Mataifa mengi na taasisi za kimataifa zinaunga mkono majadiliano. Lakini pia wanaonya wazi kwamba hawatakuwa nyuma yenu ikiwa mnashikilia uamuzi wa upande mmoja. Katika muktadha wa sasa kura ya maoni ya oktoba mosi haiwezi kuwa sababu ya kujitangazia uhuru. Lakini inaweka uwezekano wa kuanzisha majadiliano na usuluhishi wa kimataifa," amesema Colau.
Kiongozi wa upinzani cha Kisoshalisti nchini Uhispania pia ameungana na serikali kupinga uhuru wa jimbo la Catalonia. Lakini pia upinzani umetoka nje ya nchi.Waziri wa Ufaransa anayehusika na masuala ya Umoja wa Ulaya Nathalie Loiseau alisema ikiwa Wacatalonia watajitangazia uhuru basi utakuwa wa upande mmoja na kutotambulika kimataifa.
Kwa upande mwingine, chama kinachoongoza Scotland, Scottish National Party kimeunga mkono hatua hiyo na kusema serikali ya Uhispania inapaswa kuheshimu matokeo ya "Ndiyo" ya kura ya maoni iliyofanyika Oktoba mosi licha ya kupigwa marufuku na Madrid, ambapo asilimia 43 ya wapiga kura walijitokeza.
Puigdemont amesema kura hiyo ilidhihirisha watu wanataka kujitenga na wafuasi wake wanamtaka atangaze uhuru suala ambalo ni kwenda kinyume na serikali kuu na mahakama za kitaifa.
Naibu waziri mkuu wa Uhispania Soraya Saenz de Santamaria ameonya jana kwamba hatua ya kujitangazia uhuru haitaachwa hivi hivi ."Ninachoweza kusema kama watajitangazia uhuru wa upande mmoja hautakuwa na athari. Ni wajibu wa serikali ya Uhispania kupitia seneti, kwasababu nataka kukumbuka kwamba huu ni mchakato wa kisheria, wa kuchukua hatua".
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na mkuu wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker wamezungumza na waziri mkuu Mariano Rajoy kwa njia ya simu mwishoni mwa juma. Merkel amesema anaunga mkono umoja wa Uhispania na wote walibadilishana mawazo namna gani mazungumzo ya ndani ya Uhispania yanavyoweza kutekelezwa katika kwa kuheshimu misingi ya katiba.
Utafiti wa maoni uliofanywa hivi karibuni unaonyesha kwamba wacatalonia wamegawanyika kuhusu suala la kujipatia uhuru, ingawa viongozi wa mkoa wanasema vurugu za polisi wakati wa kura ya maoni zimechangia wengi kutofautiana na serikali kuu mjini Madrid.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba