Catalonia yashindwa kumchagua rais mpya
23 Machi 2018Mgombea Jordi Turull, waziri wa zamani katika serikali ya awali ya Catalonia, alishindwa kupata wingi wa kura uliohitajika kutokana na mpasuko wa vyama vitatu ambavyo vinatafuta uhuru wa jimbo hilo la kaskazini mashariki.
Kujizuia kwa wabunge kutoka chama kinachopinga ubepari cha CUP kulimuacha Turull na kura 64 wakati ambapo alihitaji 68. Sheria za bunge zinasema huenda akawa na nafasi ya pili ya kuchaguliwa siku ya Jumamosi, wakati ambapo wingi wa kutosha wa kura zaidi za "Ndiyo” kuliko za "La” utahitajika ili kumfanya kuwa rais ajaye wa Catalonia.
Lakini Turull na viongozi wengine watano wanaounga mkono kujitenga wana miadi na mahakama ya juu kabisa ya Madrid hii leo, wakati ambapo jaji huenda akawafungulia mashitaka kuhusiana na uasi na kuwaweka kwenye gereza la kuwazuia kufanya shughuli zao za kawaida.
Bunge hilo la kikanda sasa lina miezi miwili ya kumchagua rais na kuunda serikali kabla ya uchaguzi mpya kuitishwa. Wagombea wengine huenda wakazuiwa wakati huo.
Turull alipata kura za kundi lake la "Together for Catalonia” yaani "Pamoja kwa ajili ya Catalonia” na Republican Left, wakati wanachama wanne wa chama cha CUP walisusia. Wabunge 65 wa vyama vinavyotaka Catalonia kusalia kuwa sehemu ya Uhispania walipiga kura dhidi yake.
Turull tayari alimaliza mwezi mmoja kwenye gereza la kumzuia kufanya shughuli zake kama sehemu ya uchunguzi wa mahakama kuhusiana na tangazo la uhuru lililokwenda kinyume cha sheria la bunge la jimbo hilo mwezi Oktoba, ambalo lilisababisha Waziri Mkuu Mariano Rajoy kuivunja serikali ya Catalonia.
Turull ni mgombea wa tatu aliyependekezwa na wabunge wanaounga mkono kujitenga tangu waliposhikilia wingi wao mdogo wa kura katika uchaguzi wa Desemba uliotishwa na Rajoy. Msemaji wa chama cha CUP bungeni Carles Riera alisema chama chake hakingeweza kumkubali mgombea mwingine isipokuwa rais wa zamani Carles PUIGDEMONT, ambaye alikimbilia Ubelgiji mwezi Oktoba.
Riera kisha akaongeza mpasuko ndani ya kundi la vyama vinavyodai kujitenga, kwa kutangaza kuwa CUP kinavunja ushirika wake na vyama vyingine viwili.
Wakati huo huo, Mahakama ya Juu ya Uhispania imepinga ombi la kutaka waachiliwe huru viongozi wawili wakuu wanaotaka kujitenga kutoka kizuizini kabla ya kuanza kesi zao wakati jaji akichunguza jaribio la Catalonia la kutaka kujitenga. Mahakama hiyo ya juu kabisa imetoa uamuzi kuwa bado kuna hatari kuwa Joaquim Forn, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Catalonia aliyeachishwa kazi na aliyekuwa rais wa kundi la kutetea haki za raia ANC ambalo linaunga mkono uhuru wa jimbo hilo, wanaweza kurudia makossa ambayo yaliwapeleka jela.
Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Josephat Charo