1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Catherine Ashton aizuru Lebanon

Admin.WagnerD23 Oktoba 2012

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Cathrine Ashton amefanya ziara nchini Lebanon na kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa nchi hiyo Najib Mikati, yaliyogubikwa na Syria na mauaji ya mkuu wa upelelezi Wissam Hassan.

European Union Foreign Policy Chief Catherine Ashton addresses the media in Moscow, June 19, 2012. Iran and world powers failed to resolve differences over Tehran's nuclear programme on Tuesday and agreed to a technical follow-up meeting in Istanbul on July 3, Ashton said. REUTERS/Sergei Karpukhin (RUSSIA - Tags: POLITICS ENERGY)
EU-Außenbeauftragten Ashton in Moskau Nuklearprogramm IranPicha: Reuters

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Lebanon, Angelina Eichhorst alisema Ashton atamhakikishia waziri mkuu Mikati, msaada wa umoja huo katika kushughulikia wakimbizi wanaotoka Syria kwenda Lebanon. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, kuna takribani wakimbizi 67,000 wa Syria waliosajiliwa nchini Lebanon. Ziara ya Ashton inakuja wakati hali inazidi kuwa tete nchini humo, na serikali ikilaazimika kupeleka vikosi katika maeneo yanayokaliwa na waumini wa madhehebu ya sunni mjini Beirut. Jeshi lilisema limedhamiria kurejesha amani mjini Beirut, lakini mji wa bandari wa kaskazini wa Tripoli nao ulitikiswa na mapigano siku ya Jumatatu, kati ya makundi yanayomuunga na kumpinga rais Bashar al-Assad na kusababisha vifo vya watu saba.

Maafisa usalama wakibeba jeneza la mkuu wa Intelijensia, Brigedia Jenerali Wissam Hassan siku ya Jumapili. Wissam aliuawa katika shambulio la bomu mjini Beirut siku ya Ijumaa.Picha: Reuters

Lebanon ni nchi yenye dini mbalimbali ambapo Wakristu, washia na waislamu wa madhehebu ya sunni wote wanachangia theluthi moja ya raia wa nchi hiyo. Chini ya makubaliano yasiyo rasmi, rais anatakiwa kuwa mkristu wa madhehebu ya Maronite, waziri mkuu msunni na spika wa bunge mshia. Wasunni wana hasira juu ya kile wanachokiita mauaji ya serikali ya Syria dhidi ya Brigedia Jenerali Wissam Hassan, msunni ambaye alikuwa anafuatilia makosa ya Syria nchini Lebanon likwemo la mauaji ya waziri mkuu wa Lebanon Rafiq Hariri mwaka 2005. Msiba wake siku ya Jumapili ulitumika kama nafasi ya kupinga kuingilia kwa Syria katika masuala ya ndani ya Lebanon, lakini kibao kilimgeukia waziri mkuu Mikati wakimtaka ajiuzulu kutokana na kushindwa kuilinda Lebanon dhidi ya njama za Syria.

Assad atangaza msamaha Syria

Na huko Syria kwenyewe, rais Bashar al-Assad ametangaza msamaha kwa makosa yote yalitendeka nchini humo hadi wakati huu, achilia mbali yale utawala wake unaoyaita ya kigaidi, televisheni ya nchi hiyo ilisema. Assad alitangaza msamaha wa jumla wa makosa yaliyofanyika hadi tarehe 23 mwezi huu wa kumi. Msahama huo, ilisema televisheni hiyo ya taifa, ni kwa wale tu wanaojisalimisha kwa mamlaka, na si wale wanaoendelea kufanya uasi. Haikubainika wazi kama msamaha huo unahusu pia wale walioko magerezani.

Waandamanaji wakichoma picha ya rais wa Syria Bashar al-Assad wakati wa msiba wa Brigedia Jenerali Wissam Hassan. Waumini wa Sunni wanailaumu Syria kwa mauaji ya Hassan.Picha: AP

Hayo yanajiri wakati ndege za serikali zikiripotiwa kuendelea kuushambulia mji wa Aleppo licha ya matumaini ya kusitisha mapigano baadaye wiki hii. Si waasi wala serikali wanaoonekana kutaka kusitisha mapigano, na idadi ya vifo inazidi kuongezeka kupita 100 kila siku. Kiongozi wa kundi kuu la upinzani Abdelbaset Sieda amesema kuna uwezekano mdogo sana kuwa pendekezo la kusitisha mapigano linaweza kutekelezeka. Umoja wa mataifa umesema unaanda kikosi cha kulinda amani kukipeleka nchini humo endapo pande zote zitakubali kusitisha mapigano.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape, dpae, afpe,
Mhariri: Saumu Yusuf Ramadhan