1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CCM inaendelea kuongoza katika hesabu ya kura

30 Oktoba 2020

Matokeo ya uchaguzi mkuu nchini Tanzania yanaendelea kuonyesha kuwa mgombea urais wa CCM, Rais John Magufuli anazidi kuongoza huku waliokuwa vigogo katika bunge lililopita kupitia vyama vya upinzani wakipukutika.

Afrika Tansania Mosambik SADC  John Magufuli
Picha: DW/D. Khamis

Kwa mujibu wa matokeo yanayoendelea kutolewa na tume ya taifa ya uchaguzi, Rais Magufuli anayewania muhula wake wa pili na wa mwisho kwa mujibu wa katiba anaendelea kuongoza katika majimbo yote yaliyotangazwa. Matokeo hayo yanaonyesha kuwa Rais Magufuli amekuwa akiongoza katika kila jimbo kwa zaidi ya asilimia 85 hasa yale ya Tanzania bara.

Uchaguzi huu umewatupa nje ya ulingo wa siasa za bunge karibu vigogo wote wa upinzani ambao wamejikuta wakishindwa kutetea nafasi zao na hivyo kufanya bunge lijalo kutawaliwa na baadhi ya sura mpya. Mwanasiasa na aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa sera za Rais Magufuli Bungeni, Zitto Kabwe ameungana na vigogogo wengine wa upinzani waliowekwa katika kapu moja la kutorejea tena katika bunge lijalo na huenda wengi wataendelea kumkumbuka kwa umachachari wa hoja zake bungeni.

Zitto Kabwe- Kiongozi mkuu wa ACT WazalendoPicha: DW/S. Khamis

Jimbo la Arusha lililokuwa ngome ya muda mrefu ya Chadema limebadili gia na kuelekea chama tawala baada ya aliyekuwa mgombea wake, Godbless Lema kushindwa kutetea nafasi hiyo kwa mpinzani wake wa muda mrefu, Mrisho Gambo ambaye wakati fulani aliwahi kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha. Lema alikuwa moja ya wabunge walikuwa na udhubutu wa kujadili hoja bungeni zilisababisha kuzuka kwa mvutano miongoni mwa wabunge wa chama tawala na wale wa upinzani.

CCM pia imefanikiwa kutwaa jimbo la Karatu lililokuwa mikononi mwa chadema kwa miaka 25. Upinzani hadi dakika hii umefanikiwa kupata majimbo mawili tu kati ya yote yaliyotangazwa ambako mgombea wa Cuf Shemsia Mtamba amembwaga Hawa Ghasia wa CCM katika jimbo la Mtwara Vijijini naye mgombea wa Chadema, Aida Kenan ameibuka mshindi katika Jimbo la Nkasi akimdondosha mwanasiasa wa siku nyingi Ally Kesi.

Ally Kesi analiaga bunge huku akiwa ameacha mjadala mkubwa kufuatia hoja yake ya kutaka mabadiliko ya katiba ili kutoa nafasi kwa Rais Magufuli kuendelea kuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 10.

Wagombea wote wa upinzani wamekuwa wakipinga matokeo hayo katika kile wanachosema kuwepokwa visa vya udanganyifu.