1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CCM kukutana baadae mwezi huu kufuatia kifo cha Magufuli

Deo Kaji Makomba18 Machi 2021

Wakati Tanzania ikiendelea na maombolezo kufuatia kifo cha Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kilichotokea hapo jana, bado hakuna mengi yanayojulikana kuhusu kinachofanyika kumuidhinisha rais mpya.

Tansania Wahlen 2020
Picha: picture-alliance/AP Photo

Wakati Tanzania ikiendelea na maombolezo kufuatia kifo cha Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kilichotokea hapo jana, bado hakuna mengi yanayojulikana kuhusu kinachofanyika kumuidhinisha rais mpya.

Chama anachotoka hayati Magufuli, CCM kimesema kitafanya mkutano tarehe 23 mwezi huu wa Machi, lakini vile vile hakuna maelezo ya kina kuhusu kitakachojadiliwa. 

Chama cha Mapinduzi, CCM kupitia kwa katibu wake wa itikadi na uwenezi, Amprey Polepole kimetoa taarifa rasmi kuhusu kifo cha Hayati Rais Magufuli, hii leo mjini Dodoma na kusema kuwa viongozi wa Halmashauri kuu ya Chama hicho kitaifa wanatarajia kukutana Machi 23 mwaka huu huko Dar es salaam kwa ajili ya mkutano maalumu licha ya kushindwa kuweka bayana ni kitu gani kitajadiliwa katika mkutano huo.

CCM haijaweka wazi masuala watakayojadili kwenye mkutano wa Machi 23

Picha: DW/Said Khamis

Chama hicho tawala kimepata pigo kubwa kwa kuondokewa na Rais Magufuli, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wake, na wengi wanajiuliza upi utakuwa mwelekeo wa chama hicho baada ya mwenyekiti wake kuaga dunia.

Akizungumza na ldhaa hii ya Kiswahili ya DW Deus Bugahiwa ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa akiwa Mwanza Tanzania, amesema kuwa kuna changamoto kubwa inachokikabili chama cha mapinduzi katika kuangalia nani anaweza kuziba pengo lililoachwa na John Magufuli.

Wakati hayo yakijiri, kwa upande mwingine Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, wakati Akitoa Salam zake za rambirambi, amewataka wabunge wote waliokuwa katika ziara ya kikazi katika maeneo mbalimbali nchini kurejea mara moja Jijini Dodoma na kusitisha shughuli zao zote.

Ndugai ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma wakati akizungumza na wandishi wa vyombo vya habari kuhusiana na msiba huo uliotikisa Tanzania hivi sasa.

Watu mbalimbali wameendelea kutoa Salam za rambirambi kwa serikali ya Tanzania, familia ya Hayati Rais Magufuli na Watanzania kwa ujumla kufuatia msiba huo.