1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CCM yabariki uwekezaji bandari nchini Tanzania

Deo Kaji Makomba
10 Julai 2023

Halmashauri Kuu ya chama kinachotawala nchini Tanzania CCM imebariki mchakato wa makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji wa bandari kati ya Tanzania na kampuni DP world ya Dubai.

Tanzania -Dodoma -Rais Samia Suluhu Hassan
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM ambae ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu. Samia Suluhu Hassan, akiongoza kikao cha Halmashauri kuu ya CCM Taifa.Picha: CCM office

Baraka hizo za Halmashauri Kuu ya CCM, NEC, zimetolewa siku ya Jumapili mara baada ya kumalizika kwa kikao chake cha kawaida kilichoongozwa na mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, hapa jijini Dodoma.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa NEC, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema, alisema uwekezaji huo uliokumbwa na ukosoaji mkubwa ni kwa manufaa ya uchumi wa Tanzania.

Halmashauri kuu ya chama tawala CCM TaifaPicha: CCM office

"Uwekezaji huo ni utekelezaji wa vitendo wa ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025. Serikali iongoze kasi ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya uhalisia uliomo katika makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji wa bandari wa bandari," alisema  Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Sophia Mjema.

Sakata hilo la mkataba wa Bandari ya Dar es Salaam limezidi kupamba moto miongoni mwa watu wa kada mbalimbali wakiwemo wanasheria na wanasiasa, ambapo kwa muda mrefu sasa kumekuwa na mjadala mkali kuhusu undani wa mkataba huo baina ya Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, TPA, na Dubai kupitia Kampuni ya Dubai Port World.

Makubaliano ya ngazi za kiserikali yanayohusu uboreshaji na uendeshaji wa bandari nchini Tanzania tayari yameshapingwa mahakamani na wanasheria waliofungua kesi kutaka kujua uhalali wa mkataba huo.

Spika wa bunge Tanzania awaonya waandishi juu ya ripoti za uwongo

This browser does not support the audio element.

Miongoni mwa wanasheria waliofungua kesi hiyo ni Wakili Boniphace Mwabukusi anayedai kwamba, "mkataba huo ni batili", akiongeza kuwa Watanzania wengi hawakushirikishwa.

Mawakili hao wamefungua kesi hiyo Mahakama Kuu Kanda ya Mbeyadhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Katibu wa Bunge la Tanzania kwa kutuhuma za kusaini mkataba huo wa kimataifa na kuupeleka bungeni kwa ajili ya kupitishwa bila kushirikisha umma na kutoa nafasi ya kutosha kwa wananchi kutoa maoni yao.

Kwa kikao cha ngazi za juu cha chama tawala, CCM, kutoa ridhaa zake kwa makubaliano hayo, inamaanisha sasa Rais Samia ana nguvu zaidi za kisiasa ndani ya chama chake kuutetea mkataba huo. Lakini ikiwa Mahakama itakuja na maamuzi tafauti, ni jambo la kungoja na kuona.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW