1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CCM yaeleza mtumaini ya kufanya vizuri kwenye uchaguzi

George Njogopa25 Septemba 2020

Chama cha mapinduzi nchini Tanzania CCM kimetoa tathmini yake ya kampeni huku mgombea wake urais, John Magufuli akichukua mapumziko mafupi baada ya kumaliza ngwe ya pili ya kampeni zake.

Tansania Dar es Salaam | Wahlplakate
Picha: Eric Boniphace/DW

Katika tathmini yake chama hicho tawala kimetumia sehemu kubwa ya maelezo kutoa ufafanuzi juu ya hoja zinazoibuliwa na vyama vya upinzani na kusema kwamba chama hicho kina matumaini ya kufanya vizuri katika uchaguzi huu.

Katibu wa Itikadi na uenezi wa chama hicho, Humphery Polepole amewashambulia wagombea wa upinzani hasa akimlenga mgombea wa chadema Tundu Lissu akisema amekuwa akitoa taarifa za upotoshaji kuhusiana utendaji wa serikali ya CCM.

Mwanasiasa huyo ambaye hajaeleza ni lini mgombea wa chama hicho atarejea tena kwenye kampeni baada ya kuzunguka kanda za Kati na kanda ya Ziwa amedai CCM bado inaendelea kuungwa mkono na wananchi kutokana na namna kilivyotekeleza ilani yake tangu ulipofanyika uchaguzi uliopita wa 2015.

Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM Humphery Poleple (kulia).Picha: DW/Said Khamis

Wakati huu kunaendelea kushuhudua mchuano mkali wa wagombea wanaotamba kwenye majukwaa ya kampeni na kila mmoja akionyesha matumaini ya kufanya vizuri kwenye uchaguzi huu.

Mgombea wa chadema, Tundu Lissu amekuwa akitoa ukosoaji wa waziwazi kwa serikali ya CCM akisema utawala wake umeshindwa kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wananchi.

Baadhi ya mambo anayoyatilia kipaumbele iwapo ataingia madarakani ni pamoja na kutoa nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma pamoja na kutathmini upya mwenendo wa ulipaji wa kodi.

Mikutano yote ya wagombea urais wa CCM na Chadema imekuwa ikipata mwitikio mkubwa wa wananchi hali ambayo inaashiria kwamba pengine uchaguzi huu ukawa wa vuta nikuvute kama ule ulioshuhudiwa mwaka 2015.

Mwandishi: George Njogopa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW