1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CCM yatoa mwelekeo wa utawala wa awamu ya sita

18 Machi 2022

Chama tawala nchini Tanzania CCM kimetoa mwelekeo wake tangu utawala wa awamu ya sita ushike hatamu ya uongozi kikisema nchi imepiga hatua.

Chama hicho kimesisitiza kuwa, mageuzi yanayoendelea kufanywa naRais Samia Suluhu Hassan yanaakisi nia ya kuwaleta unafuu wananchi wa taifa hilo la Afrika Mashariki. 

CCM ambayo iko madarakani kwa zaidi ya miongo minne, inaamini mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani unatosha kubashiri yale yatakayoendelea kujitokeza katika siku za usoni kama vile kuwajengea uwezo wananchi katika nyanja za uchumi na kuwawezesha kupata huduma muhimu za kijamii.

Katibu wa chama hicho Daniel Chongolo aliyekutana na waandishi wa habari, ametaja vipaumbele vingine vilivyotiliwa maanani na Rais Samia ndani ya mwaka wake mmoja ikulu kuwa ni pamoja na kuleta mshikamano wa kitaifa.

Mfariji mkuu

"Kwa nafasi zake zote muheshimiwa rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania, amekuwa ni mfariji mkuu wa taifa katika, kipindi kuanzia kuondokewa na rais wa awamu ya tano mpaka sasa wenzetu wazungu wanasema comforter-in-chief, na huu ndio ulikuwa moja ya wajibu wa kwanza kabisa ambao rais Samia aliutekeleza." Alisema Daniel Chongolo.

soma Mwaka mmoja Tanzania bila Magufuli

Samia Suluhu Hassan Picha: Eric Boniphase/DW

Chama hicho kinasema kinakaribisha maridhiano ya kisiasa na kudai kinajivunia mazungumzo yaliyoanzishwa hivi karibuni kupitia baraza la vyama vya siasa ambalo liliwaleta pamoja wadau wote wa siasa waliojadiliana kuhusu  hatma ya kisiasa ya nchi.

Mkutano wa kwanza wa kihistoria ulioandaliwa na kituo cha demokrasia ambao utajadili hali jumla ya nchi na mwelekeo wa kuendesha siasa za nchi unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Rais Samia mwenyewe.

Katika mkutano wake huo wa leo, katibu Chongolo ametumia wasaa huo kuorodhesha idadi ya mambo yaliyotekelezwa ndani ya utawala wa Samia akigusia  maeneo kama yale yanayohusu ujenzi wa barabara na madaraja, utatuzi wa kero za maji, uboreshaji wa huduma za afya na elimu. Amesema hayo yote yametelelezwa kwa ufanisi.

soma ''Lazima tukope '' asema Rais Samia

Wanafunzi wote shuleni

"Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu wanafunzi wa kidato cha kwanza wote wameingia shule kuanza masomo yao kwa siku moja, bila ya kuwepo waliosubiria nyumbani kujiunga na sekondari kwa chaguo la pili la tatu na la nne kama ilivyokuwa huko nyuma, ambalo miaka yote ilikuwa inasabishwa na mahitaji maalum au upungufu wa miundo mbinu." Daniel Chongolo.

Picha: Veronica Natalis/DW

Hata hivyo, chama hicho hakikugusia bayana suala la kupungua kwa huduma ya nishati ya umeme licha kwamba kumekuwepo na mradi wa ujenzi wa bwawa la Nyerere ambao ulitajwa ungeanza uzalishaji wake mapema mwaka huu. soma Ujerumani: Mradi wa umeme wa Tanzania wapigiwa kura bungeni

Katika miezi ya hivi karibuni kumekuwa na kilio kikubwa cha wananchi walioshuhudia hali ya upatikanaji umeme ikiwa dhaifu na serikali ilisisitiza hali hiyo ilisababishwa na mambo mawili, ukame na uchakavu wa mitambo.

Utawala wa Rais Samia tayari umetoa mwelekeo wa bajeti yake mpya ya mwaka huu inayokadiriwa kufikia a trilioni 41, huku lakini deni la taifa likifikia trilioni 68.

 

George Njogopa; DW Dar es Salaam

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW