1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CDU chapata matokeo mabaya katika uchaguzi wa Hesse

Caro Robi
29 Oktoba 2018

Chama cha Kansela wa Ujerumani Angela Merkel cha Christian Democratic Union CDU na chama mshirika katika serikali ya mseto ya Ujerumani cha Social Democrats SPD vimepata pigo kubwa katika uchaguzi wa jimbo la Hesse.

Berlin: CDU-Spitze berät über den Hessen-Wahlkampf
Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

CDU kimepata asilimia 27 ya kura, hayo yakiwa matokeo mabaya zaidi kwa chama hicho katika jimbo la Hesse tangu mwaka 1966 huku chama cha SPD kikipata asilimia 19.8.

Chama cha walinda mazingira cha kijani kimejinyakulia asilimia 19.8 huku chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative für Deutschland AfD kikipata asilimia 13.1 na hivyo kukiwezesha kwa mara ya kwanza kuingia katika bunge la jimbo hilo la Hesse.

AfD kinachopinga wahamiaji nchini Ujerumani,  sasa kina uwakilishi katika majimbo yote 16.

Kiongozi wa AfD Joerg MeuthenPicha: Reuters/R. Orlowski

AfD sasa kina uwakilishi katika majimbo yote 16

Chama hicho chenye misimamo mikali kilianzishwa miaka mitano iliyopita kwa misingi ya kuwapinga wahamiaji nchini Ujerumani na kimekuwa kikipata uungwaji mkono kutoka kwa wapiga kura wanaokerwa na sera za Merkel kuhusu uhamiaji.

Mmoja wa viongozi wa AfD Joerg Meuthen baada ya matokeo ya uchaguzi huo wa Jumapili wa Hesse amesema kuwa chama hicho kimetimiza malengo yake yote ya uchaguzi.

Suala hilo tete limekuwa likimzonga tangu 2015 aliporuhusu zaidi wa wahamiaji na wakimbizi milioni moja kuingia nchini humo.

Matokeo hayo mabaya kwa Merkel na chama chake cha CDU kinaendelea kuibua maswali kuhusu mustakabali wa siku za usoni wa kiongozi huyo ambaye ameingoza Ujerumani kwa miaka 13.

Katibu mkuu wa CDU Annegret Kramp-Karrenbauer ambaye anaonekana kuwa mrithi wa Merkel amesema ni uchungu mno kwa CDU kupoteza kura nyingi na ametoa wito wa kukoma kwa mivutano ndani ya chama hicho.

Merkel anatarajiwa Jumatatu saa saba mchana kuzungumzia matokeo ya uchaguzi huo wa Hesse unaokuja wiki mbili baada ya ule wa jimbo la Bavaria. Ana kibarua kigumu cha kwanza kuwashawishi SPD kusalia katika serikali ya mseto.

SPD chatafakari hatma yake 

Kiongozi wa SPD Andrea Nahels amesema hali ilivyo sasa serikalini haikubaliki na kukitaka chama cha CDU kutoa mkakati ulio wazi na madhubuti wa kisiasa utakaoweka mbele maslahi ya raia.

Kiongozi wa SPD Andrea NahlesPicha: Reuters/H. Hanschke

Nahles amesema sharti mambo yabadilike katika chama cha SPD akiongeza wanahitaji kuwa wazi kuhusu wanachokisimamia na kuitaka serikali ya mseto kuweka pamoja mkakati na kuutekeleza kabla ya mazungumzo yanayotarajiwa mwaka ujao ambapo vyama vinavyounda serikali ya mseto vitaamua iwapo viendelee kusalia katika serikali hiyo.

Idadi ya wanachama wa SPD wanaokitaka chama hicho kujiondoa kutoka serikali ya mseto na kujiunga na upinzani mara moja inaongezeka, na hivyo kuzua wasiwasi kuwa huenda Ujerumani ikashuhudia uchaguzi mkuu wa mapema.

SPD kimesema ifikapo Septemba mwaka ujao kitaweza kuona kama bado serikali ya sasa ya mseto ni sehemu sahihi kwao, kauli inayoonekana kuwa kitisho kwa Kansela Merkel.

Merkel pia ana kibarua cha kukiunganisha chama chake ambacho kinaonekana kugawika huku wanachama wengi wakizidi kutilia shaka uongozi wake.

Serikali ya mseto mara mbili nusura isambaratike, kutokana na tofauti kati ya Merkel na kiongozi wa chama ndugu cha Christian Social Union CSU Horst Seehofer kuhusu suala tete la uhamiaji.

Mwandishi: Caro Robi/AFP/Dpa

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW