1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CDU yashinda Berlin, lakini iko hatihati kuunda serikali

13 Februari 2023

Chama cha Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, cha Social Democratic, SPD, kimepta pigo katika uchaguzi wa jimbo la Berlin, kikishindwa na chama cha upinzani cha CDU jimboni humo kwa mara ya kwanza katika miaka zaidi ya 20.

Wiederholungswahl Berlin - CDU-Wahlparty
Picha: Sebastian Christoph Gollnow/dpa/picture alliance

Wakati kura hiyo ya Berlin ilijikita kwenye masuala ya ndani, pigo hilo kwa chama tawala linakuja wakati ambapo kansela Scholz anakabiliwa na ukosoaji mkubwa kutokana na kusitasita katika utoaji wa msaada wa kijeshi kwa Ukraine kufuatia uavmizi wa Urusi mwaka uliopita.

Katika uchaguzi huo uliorudiwa kwa amri ya mahakama kutokana na mapungufu yaliojitokeza kwenye uchaguzi wa mwaka 2021, chama cha kansela kimepata matokeo yake mabaya zaidi ya baada ya vita katika mji mkuu, ambako wameshikilia ofisi ya meya tangu 2001.

Chama cha CDU, kilichoko upinzani katika mji mkuu na serikali ya shirikisho, kimeongeza kura zake hadi asilimia 28 kutoka 18 kilizopata mwaka 2021. Chama cha Kijani kinaonekana kubakisha mgao wake wa kura kwa kati ya asilimia 18.4 hadi 18.5, kikiwa mbele kidogo ya chama cha Social Democratic, kilichopata asilimia 18.4 ya kura.

Soma pia: Meya wa Istanbul ziarani Berlin

Mgombea mkuu wa CDU, Kai Wegner ameyataja matokeo ya uchaguzi huo kama mafanikio ya kustajabisha, akisema "lengo letu ni kuunda serikali imara."

Meya wa sasa wa Berlin Franziska Giffey (kushoto) na mgombea umeya wa chama cha Kijani Bettina Jarasch wakiwa katika mahojiano baada ya matokea ya uchaguzi kutangazwa.Picha: Fabian Sommer/dpa/picture alliance

Meya wa Berlin Franziska Giffey, kutoka chama cha SPD, alitambua ushindi wa CDU, lakini alisema lengo lake linasalia kuongoza serikali ya muungano chini ya uongozi wa SPD, akiahidi pia kujaribu kuunda wingi imara wa kisiasa kwa ajili ya kufanikisha lengo hilo.

"Bado hatujapoteza matumaini, tunatamani kwamba SPD inapata nafasi ya pili na tunaweza kuunda muungano chini ya uongozi wa SPD katika mazingira haya ya kisiasa," alisema Giffey.

Nafasi ya kuunda serikali bado iko wazi sana

Mpaka sasa ni vigumu kujua namna serikali ya mji huo mkuu itakapoundwa baada ya kura ya jana. Chama cha CDU huenda kisifanikiwe kumuingiza Wegner katika nafasi ya meya, au hata kuhakikisha chama hicho ni sehemu ya serikali ya mji, licha ya ushindi wake.

Hii ni kwa sababu katika uchaguzi wa Ujerumani, chama kinachopata kura nyingi zaidi siyo kinachoishia kuendesha serikali wakati wote. Ukiondoa wingi wa kujitosheleza, ambao ni jambo la nadra na halijatokea Berlin, vyama vinapaswa kutafuta washirika ili kufikia wingi wa viti bungeni.

Soma pia:CDU yashinda kwa kishindo uchaguzi wa jimbo la NRW-Ujerumani 

Mjini Berlin idadi inayohitajika kudhibiti serikali ya jimbo ni viti 66 na kuna njia nyingi ambazo vyama tofauti vinaweza kuvuka kizingiti hiki.

Serikali ya sasa inayoongozwa na Giffey na washirika wake wa vyama vya Kijani na die Linke, inaweza kuendelea kuwepo. Hata hivyo ikiwa chama cha Kijani kitabakia mbele ya SPD, basi Giffey atapoteza kazi yake ya umeya.

Kwa hivyo suala la nani ataendesha jiji hilo, ambalo linakabiliwa changamoto za kodi kubwa, uhaba wa nyumba, shida za usafiri na wimbi la wakimbizi, bado halijapatiwa jibu.

Mgombea umeya wa chama cha CDU Kai Wegner akiwahutubia wafuasi wake baada ya kutangazwa kwa mataokeo ya awali ya uchaguzi wa jimbo la Berlin.Picha: Michele Tantussi/REUTERS

Meya kutoka watetezi wa mazingira?

Chama cha Kijani, katika mahojiano ya televisheni Jumapili usiku, walisema mara kwa mara kwamba wanapendelea kuendeleza muungano wa sasa.

Kwa hivyo ikiwa wataishinda SPD kwa nafasi ya pili na kushika nafasi ya pili nyuma ya CDU, na kubakisha muungano wa sasa, meya mpya atakuwa Bettina Jarasch, mgombea umeya wa Green. Die Grüne pia inaweza kuunda muungano na CDU.

Hata hivyo, wahafidhina walisababisha tafrani kati yao wakati wa kampeni ya uchaguzi, na Wegner anakabiliwa na vita kali ili kurekebisha mambo na chama cha watetezi wa mazingira.

Wegner, ambaye alipata kura nyingi zaidi, atakuwa na nafasi ya kwanza kuunda serikali na amesema atazungumza na SPD na Kijani.

Nini kilisababisha kufutwa kwa uchaguzi wa awali?

Uchaguzi huo mpya ulifanyika kwa Baraza la Wawakilishi la Berlin na vyombo vya uwakilishi vya wilaya 12 za jiji hilo, baada ya Mahakama ya Kikatiba ya Berlin kutangaza kuwa uchaguzi uliopita ulikuwa batili kwa sababu ya "dosari kubwa za kimfumo."

Katika kura ya 2021, vituo vingi vya kupigia kura havikuwa na karatasi za kutosha au zisizo sahihi na watu walilazimika kupanga foleni kwa masaa mengi.

Ziara ya waandishi wa DW kuripoti uchaguzi wa Ujerumani

01:36

This browser does not support the video element.

Upigaji kura uliendelea hadi jioni na kuendelea katika maeneo mengi hata baada ya muda ambao vituo vya kupigia kura vilipangiwa kufungwa na utolewaji wa matokeo ya awali.

Hiyo ilikuwa kwa sababu uchaguzi wa Septemba 26, 2021 ulifanyika kwenye kalenda iliyojaa matukio, kama uchaguzi wa shirikisho, kura ya maoni kuhusu kuzinyang'anya kampuni kubwa za nyumba majumba yao na mbio ndefu za Berlin Marathon vyote, vilifanyika tarehe hiyo hiyo.