1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CDU wapata ushindi mkubwa Saxony-Anhalt

7 Juni 2021

Chama cha Kansela Angela Merkel wa Ujerumani cha CDU kimepata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwisho wa mikoa kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wa kwanza katika miaka 16 bila kumhusisha kansela huyo mkongwe

Landtagswahl Sachsen-Anhalt - CDU
Picha: Bernd Von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Matokeo ya mwanzo yanaonyesha kuwa chama cha CDU chini ya kiongozi mpya Armin Laschet kimeshinda karibu asilimia 37 ya uchaguzi wa jimbo la Saxony-Anhalt, dhidi ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia AfD katika nafasi ya pili na asilimia 21.

Chama cha wanamazingira cha Kijani, ambacho hadi hivi karibuni kilikuwa na ushindani mkali na CDU na chama chake ndugu cha Bavaria cha Christian Social Union – CSU katika ngazi ya kitaifa, kilipata matokeo mabaya ya karibu asilimia 6 ya kura.

Soma pia: Uchaguzi wa jimbo la Saxony-Anhalt mtihani kwa chama cha CDU

Ushindi huo wa CDU chini ya waziri mkuu wa Saxony-Anhalt Reiner Haseloff unaonyesha ongezeko la asilimia 7 tangu uchaguzi wa mwisho 2016. "Watu wa Saxony-Anhalt wametuma ujumbe wa wazi leo. Mkoa wa Saxony-Anhalt unabaki imara katika kitovu cha siasa. Wapiga kura wameamua kuwa Reiner Haseloff ataendelea kuwa Gavana wa Jimbo na kuliongoza jimbo hili zuri kwa siku zijazo. CDU ina wajibu wa wazi wa kuongoza. Sisi ndio chama chenye nguvu kubwa kisiasa na matokeo yetu leo ni mazuri sana." Amesema Paul Ziemiak ni katibu mkuu wa CDU

Armin Laschet, mkuu wa chama cha CDUPicha: Marcel Kusch/REUTERS

Chama cha Merkel CDU kwa miaka mingi kimekua nguvu kubwa katika jimbo la Saxony-Anhalt la iliyokuwa Ujerumani Mashariki, kwa kushinda uchaguzi wote wa eneo hilo isipokuwa mmoja tu tangu kuungana kwa Ujerumani mbili mwaka wa 1990.

Laschet ambaye aliteuliwa kuwa mgombea wa kihafidhina wa wadhifa wa ukansela mwezi Aprili, alirithi mfululizo wa matatizo ikiwemo hasira kuhusiana na namna serikali ililishughulikia janga la corona na kashfa ya rushwa inayohusisha kandarasi za mashaka za barakoa za kuzuia virusi vya corona

Katika uchaguzi wa mwisho wa mikoa mwezi Machi, katika majimbo ya Rhineland Palatinate na Baden-Wüttemberg – CDU ilipata matokeo mabaya kabisa katika majimbo hayo.

Laschet mwenyewe alikuwa ameathirika na umaarufu mdogo, kufuatia malumbano ya ndani wahafidhina kuhusu uteuzi wa mgombea wa ukansela. Lakini mambo yamebadilika Ujerumani katika wiki za karibuni wakati kampeni ya chanjo ya corona nchini ikishika kasi na maeneo makubwa ya nchi kufunguliwa tena baada ya kufungwa kwa miezi kadhaa.

Kiongozi upande wa Wanamazingira Annalena Baerbock, mafanikio ya CDU yalitokana na wapiga kura kutaka kukizuia chama cha AfD. Amesema wengi walikipigia CDU kwa sababu hawakutaka kuwaona serikalini viongozi wa itikadi kali za mrengo wa kulia

AFP/AP/Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW