1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CDU yanyakua ushindi Saarland

3 Aprili 2017

Hatimae uchaguzi wa jimbo la Saarland umemalizika na chama cha Kansela Angela Merkel cha Christian Demokratik Union (CDU) kimeibuka na ushindi hivyo basi kukishtua chama cha Social Demokratik (SPD).

Landtagswahl Saarland Annegret Kramp-Karrenbauer
Picha: picture alliance/dpa/P.Dietze

Mwaka wa uchaguzi mkuu nchini Ujerumani ulianza hapo jana kwa uchaguzi katika jimbo la dogo kabisa la Saarland la magharibi mwa nchi ambapo wapiga kura laki nane walipiga kura kuwachagua wabunge.  Uchaguzi huo ni wa kwanza kufanyika wa majimbo ya Ujerumani kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi Septemba mwaka huu.

Chama cha kihafidhina cha kansela Angela Merkel cha Christian Demokratik Union(CDU) kilipata ushindi wa kuridhisha dhidi ya washindani wake wa chama cha Social Demokratik (SPD).  Chama cha CDU kilipata asilimia 40.7 huku chama cha SPD kikipata asilimia 29.6 katika uchaguzi huo uliofanyika katika jimbo hilo linalopakana na Ufaransa.

Mwenyekiti wa chama cha SPD Martin SchulzPicha: picture alliance/dpa/M.Tantussi

Kwa upande wake chama cha Social Demokratik kimepata pigo kutokana na kushindwa kwake katika uchaguzi huo wa jana hasa kutokana na chama hicho kujiimarisha katika kipindi cha  muda mfupi tangu Martin Schulz kuchukuwa nafasi ya uongozi wa chama hicho.

Mjumbe mmoja wa ngazi ya juu katika chama cha  CDU amesema chama hicho cha kihafidhina kilipata ushindi kwa asilimia zaidi ya kilivyotegemea na kwamba hatua hiyo inakipa matumaini chama hicho ya kuweza kuibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao. Katibu mkuu wa chama hicho cha CDU Peter Tauber amesema chama cha CDU ndio chama pekee cha kisiasa kinachojipambanua na vyama vyenye kulemea mrengo mkali wa kushoto na kulia vinavyotafuta umaarufu kwa kutumia hoja za kijuu juu.  Kansela Merkel ambaye ni mwenyekiti wa chama cha CDU amesema uchaguzi ni swali juu ya nani anayeweza kuleta mustakabali mzuri zaidi na jibu wanalo wapiga kura. Akizungumzia juu ya uchaguzi wa jana mwenyekiti mpya wa SPD Martin Schulz ambaye pia ni mgombea wa ukansela amesema hawakulifikia lengo lao katika jimbo la Saarland lakini haina maana kwamba hawatalifikia lengo lao kuu la kuibadilisha serikali ya Ujerumani.

Katika uchaguzi wa jana vyama vilivyo anguka ni chama cha walinzi wa mazingira kilichopata asilimia asilimia 4.0, chama hicho cha kijani kilishindwa kufikia asilimia tano ya kura ili kuweza kuingia bungeni.  Chama cha mrengo mkali wa kulia kinachoitwa chama mbadala kwa Wajerumani AfD kimefanikiwa kuingia katika bunge la jimbo la Saarland kwa kupata asilimia 6.2 ya kura.

Mwandishi: Zainab Aziz DPAE/APE/DW

Mhariri:Yusuf Saumu

  

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW