1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CENI yatoa mwito kwa Kanisa kuuhamamisha umma juu ya kura

Jean Noël Ba-Mweze
22 Desemba 2022

Zoezi la kuwaandikisha wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Disemba, 2023 Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo linatarajiwa kuanza siku ya Jumamosi.

Niger | Präsidentschaftswahlen in Zinder
Picha: Mohamed Tidjani Hassane/DW

Zoezi la kuwatambua na kuwaandikisha wapiga kura litachukuwa muda wa mwezi moja katika kila eneo. Eneo la kwanza ambapo shughuli hiyo itaanzishwa Jumamosi linajumuisha mikoa 10, ambayo ni Kongo ya Kati, Kinshasa, Kwango, Kwilu, Maï-Ndombe, Ekwatori, Mongala, Ubangi Kaskazini na Kusini, pamoja na Tshuapa.

Tume Huru ya Uchaguzi, CENI imewataka wapiga kura kujitokeza kwa wingi na hivyo, imetoa wito kwa Kanisa Katoliki kushiriki katika uhamasishaji. Didi Manara, makamu wa pili wa mwenyekiti wa CENI amesema, "Unajua Kanisa Katoliki ni kanisa kubwa la kwanza kabisa katika eneo la taifa na kwa hiyo likituacha itakuwa balaa. Lakini tunafurahi sana. Leo ni siku kubwa kabisa kwa tume ya uchaguzi kuwa na uhakika wa Kanisa Katoliki kuhusu uhamasishaji wa wapiga kura."

Kanisa Katoliki limekubali wito huo wa kuhamasisha umma

Baadhi ya wapiga kura wakionyesha karatasi za kura zinazodaiwa kujazwaPicha: dapd

Kanisa katoliki lilijiondoa katika shughuli za uchaguzi baada ya kuteuliwa Denis Kadima kama mwenyekiti wa CENI. Lakini limekubali wito huo na kuahidi litajitolea kuwahamasisha waumini wake, ingawa haitakuwa rahisi kwani Wakongo tayari wamepoteza imani katika uchaguzi,.

Askofu Donatien Tshole, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki wa Kongo, CENCO anaeleza, "Ukweli ni kwamba Wakongo wengi hawana tena imani na mchakato wa uchaguzi. Halafu kuwaalika kwenye uchaguzi ni lazima kwanza wapewe sababu za kuamini kuwa utakuwa tofauti na uchaguzi uliopita. CENI ilidhamiria kutangaza matukio ya kila kituo cha kupigia kura na hilo linaweza kuwahakikishia Wakongo kwamba haitakuwa kama zamani."

Soma pia: Kongo imefikia wapi katika kupambana na rushwa ?

Wakati hayo yakijiri, wanaharakati wa mashirika ya kiraia wameelezea wasiwasi wao kufuatia jinsi watu wengi watatumia darubini moja kwa sampuli ya jicho, katika nchi ambapo kumerikodiwa tena visa vya COVID-19.

Wakionya kwamba hiyo inaweza kusambaza magonjwa mengi, wamemtumia Rais Félix Tshisekedi barua, kama alivyothibitisha Dieudonné Mushagalusa, mratibu wa mashirika hayo. "Wasiwasi huu ulitusukuma kumuandikia rais barua kwani kuwatambua wapiga kura kwa jicho kunaweza kusambaza virusi vya corona pamoja na magonjwa mengine. CENI haikuonya wala kutoa taarifa yoyote. Na hivyo tumeamua kumjulisha rais wa Jamhuri ili aweze kuwatuliza Wakongo."

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaanda uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 20 Disemba mwaka 2023 na kujumuisha uchaguzi wa rais, wa bunge la kitaifa na la mikoa, pamoja na washauri wa manispaa.