1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CENI yatuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha

Saleh Mwanamilongo
16 Januari 2024

Ripoti ya mashirika ya kiraia, imesema Tume huru ya Uchaguzi, CENI, imeshindwa kuelezea matumizi ya dola milioni 400 ilizopokea na kutoa kandarasi za manunuzi zisizo wazi katika maandalizi ya uchaguzi wa Desemba 20.

DR Kongo Kinshasa 2023 | Makao Makuu ya CENI
Tume huru ya Uchaguzi nchini Kongo, CENIPicha: Saleh Mwanamilongo/DW

Ripoti hiyo imesema tume ya uchaguzi nchini Kongo CENI pia ilikumbwa na ongezeko kubwa la bajeti, suala ambalo limekuwa likiusumbua utawala wa Rais Felix Tshisekedi.

Ripoti hiyo ya kurasa 52 imeitaka mahakama ya Kongo kufungua mara moja uchunguzi juu ya usimamizi wa fedha za umma ilizotengewa CENI kwa ajili ya mchakato wa uchaguzi. Dieudonné Mushagalusa mratibu wa mashirika ya kiraia nchini Kongo ameunga mkono pendekezop hilo.

''Ni jambo la aibu kubwa kuona fedha za umma zimefujwa na kutumika kiholela kama watu wanaogawanya karanga. Ni lazima idara za mahakama kufungua uchunguzi kwa sababu ni jambo lisilo kubalika ikitizamwa jinsi uchaguzi ulivyoandaliwa, licha ya hiyo mpaka sasa mawakala wa tume ya uchaguzi hawajalipwa mishahara yao,'' alisema Dieudonné Mushagalusa

Umoja wa Mataifa wakubali kuisaidia Congo katika usafirishaji wa vifaa vya kura

Valery Madianga, mmoja ya waandishi wa ripoti hiyo amesema mtiririko wa matumizi ya fedha hizo hauko wazi, na hiyo bila shaka inaathari matokeo ya uchaguzi.

Madianga amesema fedha za umma zimetumika vibaya sana, au labda zimeingia kwenye mifuko isiyoeleweka. Ripoti hiyo pia ilisema kuwa kandarasi 45 kati ya 54 za umma zilizosainiwa na tume ya uchaguzi zilitolewa bila kufuata sheria, na kandarasi tisa pekee ndizo zitolewa kupitia zabuni.

Upinzani wataka uchaguzi urudiwa

Wagombea wa uchaguzi katika uchaguzi wa DRC Kongo Desemba 20. Felix Tshisekedi Moise Katumbi, Denis Mukwege na Martin Fayulu Picha: AFP/Getty Images, picture alliance, G. Kusema, DW

Kasoro za kiufundi, ukosefu wa vifaa katika dakika za mwisho siku ya uchaguzi na kuongezwa muda wa upigaji kura kinyume cha sheria ni baadhi ya changamoto zilizoukumba uchaguzi wa rais na bunge uliotishwa Desemba 20.

Wagombea wakuu wa upinzani walilalamikia maandalizi mabaya na udanganyifu wa kura na kutaka uchaguzi huo urudiwe.

Ripoti hiyo iliotolewa na Kituo cha Utafiti wa matumizi ya Fedha za Umma na Maendeleo ya Mitaa (CREFDL) kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya, ilisema tume ya uchaguzi ilipokea karibu dola bilioni 1.1 kati ya 2021 na 2023 kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi.

Lakini ni dola milioni 711 pekee zilizoidhinishwa katika kufadhili uchaguzi, na kuacha takriban dola milioni 400 kutojulikana matumizi yake. Tume ya uchaguzi na serikali ya Kongo havikutoa maelezo yoyote na hawakujibu ombi la waandishi habari la kutaka ufafanuzi.

Mwandishi : Saleh Mwanamilongo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW