1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBurkina Faso

Chad na Mauritania zafungua njia ya kufutwa muungano wa G5

Admin.WagnerD7 Desemba 2023

Wanachama wawili waliobaki wa Muungano wa Afrika Magharibi wa nchi tano za ukanda wa Sahel zinazojulikana kama G5 wamesema wanajiandaa na kufungua njia ya kuuvunja muungano wa kiusalama wa kundi hilo.

G5 Sahel
Jenerali Oumarou Namata Gazama, mkuu wa kikosi cha pamoja cha G5 Sahel.Picha: Michele Cattani/AFP/Getty Images

Kundi hilo lilioanzishwa ili kupambana na uasi wa wapiganaji wenye itikadi kali. Hatua hii imechukuliwa ni baada ya nchi nyingine tatu waasisi kujiondoa. 

Muungano wa G5 Sahel, ambao unazijumisha pamoja nchi za Mauritania, Chad, Burkina Faso, Mali na Niger, uliundwa mnamo 2014 na siku ya Jumamosi, Burkina Faso na Niger zilitangaza kuwa zinajiondoa kutoka kwa muungano huo. Mwaka jana jeshi la Mali lilitangaza kujiondoa.

Soma pia:Kundi la G5 kuvunjwa rasmi 

Chad na Mauritania zimesema katika taarifa kuwa zinafahamu na kuheshimu uamuzi wa uhuru wa Burkina Faso na Niger kuondoka katika muungano huo wa kijeshi, zikifuata nyayo za Mali.

Aidha, mataifa hayo mawili yamesema yatatekeleza hatua zote muhimu kwa mujibu wa mkataba wa muungano huo hasa kifungu cha 20 ambacho kinasema kuwa muungano huo unaweza kuvunjwa kwa ombi la angalau nchi tatu wanachama.

Licha ya kutangaza kujiondoa kwao siku ya Jumamosi, viongozi wa kijeshi wa Burkina Faso na Niger hawakutoa wito wa wazi wa kutaka muungano huo uvunjwe, lakini hatma ya kundi hilo ilionekana kufifia hata kabla ya jeshi la Mali kutangaza kujiondoa mnamo 2022.

Mafaniko ya Muungano huo

Jeshi la Ufaransa katika operesheni za kijeshi kaskazini mwa Burkina FasoPicha: Michele Cattani/AFP/Getty Images

Kikosi cha pamoja cha kijeshi kimepata matokeo kidogo tu kimsingi, operesheni chache za pamoja za G5 zimefanyika na hali ya usalama imeendelea kuzorota.

Soma pia:Viongozi wa G5 wafanya mkutano kujadili vita dhidi ya ugaidi

Ghasia zimeenea na maelfu ya raia na wapiganaji wameuawa na mamilioni ya watu kuyahama makaazi yao na kuchangia katika kukosekana kwa utulivu wa kisiasa katika ukanda huo, ambao umeshuhudia mfululizo wa mapinduzi ya kijeshi kama vile nchini Mali mwaka 2020, Burkina Faso mwaka 2022 na mapema mwaka huu nchini Niger.

Taarifa ya pamoja kutoka Burkina Faso na Niger iliyosomwa na mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Burkina Faso, RTB imesema::

''Muungano unapata changamoto kufikia malengo yake. Kibaya zaidi ni kwamba matamanio halali ya mataifa yetu ya kuifanya G5 Sahel kuwa eneo la usalama na maendeleo yanazuiwa na vikwazo vya kitaasisi na mizigo ya kizamani ambayo inatuaminisha kwamba njia ya uhuru na utu ambayo tunaipitia sasa inaenda kinyume na sheria na ushiriki katika G5 Sahel katika hali yake ya sasa."

Mwaka wa 2017, viongozi wa nchi hizo tano walikubaliana kuunda kikosikazi cha pamoja cha kupambana na ugaidi kikiungwa mkono na Ufaransa. Lakini watawala wa kijeshi wa Burkina Faso, Niger, na Mali wote wameituhumu Ufaransa kwa kuwa na jukumu la kupitiliza baada ya miaka mingi ya kupelekwa vikosi vya Ufaransa kwenye nchi hizo.