Chad yataja serikali mpya ya mpito
3 Mei 2021Aidha, Utawala wa kijeshi umeahidi kurejesha demokrasia kwenye taifa hilo la ukanda wa Sahel.
Kulingana na msemaji wa jeshi Azem Bermandoa, Baraza la Kijeshi la Mpito (CMT) linaloongoza kwa sasa limeahidi kurejesha demokrasia katika kipindi cha miezi 18 baada ya kile ambacho upinzani ulikitaja kama mapinduzi ya kitaasisi.
Bermandoa amesema kupitia hotuba ya televisheni kwamba rais Mahamat Deby mtoto wa rais Deby ameitangaza serikali hiyo yenye mawaziri 40 pamoja na manaibu na kuunda wizara ya maridhiano ya kitaifa itakayoongozwa na Acheick ibn Oumar aliyekuwa kiongozi wa waasi, ambaye mwaka 2019 alichaguliwa mshauri wa rais wa masuala ya diplomasia.
Mpinzani mwingine mwandamizi Mahamat Ahmat Alhabo ataongoza wizara ya sheria. Wengi wa mawaziri kwenye serikali hii ya mpito hata hivyo wanatokea kwenye serikali iliyopita.
Upinzani wasisitiza kuzingatiwa matakwa ya raia.
Kiongozi wa upinzani Success Masra ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba hii haitawafikisha kokote iwapo hawatarejea kwenye misingi inayozingatia matakwa ya wananchi, ambayo ni kuwa na rais wa kiraia, na makamu kutoka jeshi. Amesema uteuzi huo unatoa taswira ya ujenzi wa nyumba unaoanzia kwenye paa.
Chad imejikuta katika mzozo baada ya kifo cha Idriss Deby kilichotangazwa siku moja tu baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa Aprili 11 ambapo alikuwa aongoze kwa muhula wa sita.
Jeshi limesema watu sita wamekufa wiki iliyopita kufuatia maandamano ya kuupinga utawala wa kijeshi katika mji mkuu N'Djamena na eneo la kusini, ingawa wanaharakati wa haki za binaadamu wanasema ni watu tisa.
Kwenye maziko ya wahanga hao yaliyofanyika siku ya Jumamosi, mwanaharakati wa haki za binaadamu Serge Ngardji alipomzungumzia mwandamanaji Djigolem Yannick, aliyeuawa kwenye maandamano hayo alisema wataendelea kupigania haki zao katika kuhakikisha kizazi kijacho kinakuwa na maisha bora.
Amesema "Tutaendeleza mapambano, tutaendeleza ili kujitoa kwetu kusiwe kazi bure. Lazima tuendelee kupambana ili maisha ya kesho ya ndugu zetu yawe mazuri. Lazima tuendelee kupambana ili kesho ya ndugu zake wawe na maisha mazuri ama hata wapate fursa ya kwenda shule na kutibiwa. Kwa hivyo tutaendelea ili kuwe na uhuru."
Zaidi ya watu 650 wanashikiliwa na jeshi la polisi kufuatia maandamano hayo yaliyozuiwa na mamlaka. Aidha, hapo jana jeshi liliondoa kizuizi cha kutotoka nje usiku kilichotangazwa baada ya kifo cha rais Deby.
Mashirika: RTRE/AFPE