1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chad yavunja uhusiano na Sudan

Rahab Fred14 Aprili 2006

Rais wa Chad, Idriss Deby ametangaza kuwa serikali yake imevunja uhusiano wote wa kidplomasia na Sudan na amewaamuru wanadiplomasia wa nchi hiyo waondoke Chad.

Rais wa Chad, Idriss Deby
Rais wa Chad, Idriss DebyPicha: AP

Rais Deby ameitangaza hatua hiyo baada ya waasi wa United Front for Change-FUC, ambao anadai wanasaidiwa na Sudan, kuuvamia mji mkuu wa Chad, Ndjamena wakiwa na azma ya kumuondosha madarakani kiongozi huyo aliyetawala kwa kipindi cha karibu miaka 16. Hata hivyo Sudan imezikanusha tuhuma hizo za kuwasaidia waasi wa Chad.

Rais Deby atashiriki kwenye uchaguzi mkuu nchini humo utakaofanyika tarehe tatu mwezi ujao.

Rais huyo wa Chad, amesema pia atawafukuza wakimbizi wote laki mbili waliopewa hifadhi nchini Chad, ikiwa Umoja wa mataifa na Umoja wa Afrika hawataisaidia nchi hiyo kutatua mzozo wa kile anachokitaja kuwa ni jaribio la Sudan la kuvuruga amani ya Chad.

Amesema pia jumuiya ya kimataifa haina budi kuutafutia ufumbuzi mzozo wa jimbo la Darfur nchini Sudan kuanzia sasa ili wakimbizi waliopo Chad warejee kwao Sudan, kwa sababu kuanzia mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu Chad haitatoa hifadhi kwa wakimbizi wa Sudan.

Hapo jana waasi walipambana vikali na wanajeshi wa Chad kwenye mji wa Ndjamena lakini leo vurugu hizo zimedhibitiwa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika yameyalaumu mashambulio ya jana ya waasi kwenye mji wa Ndjamena na pia mabaraza hayo yamezitaka Chad na Sudan zichukue hatua za kuutatua mzozo baina yao.

Waziri anayeshughulikia masuala ya Chad, Mahamat Ali Abdallah, hii leo amesema takribani waasi 370 na wanajeshi 30 wa Chad wameuawa wakati wa ghasia hizo.

Waziri huyo pia amesema karibu wanajeshi 100 walijeruhiwa wakati wa mapambano na waasi wa FUC, na waasi 287 wanashikiliwa na wanajeshi wa Chad.

Leo katika eneo la wazi la jengo la bunge la Chad, wanajeshi wa nchi hiyo wamewaweka waasi waliokamatwa na kuzionyesha pia maiti za waasi waliouawa wakati wa wakipambana nao, ili kudhihirisha ushindi walioupata dhidi ya waasi hao.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW