CHADEMA: Heche afunguliwa mashtaka ya ugaidi
5 Novemba 2025
Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho iliyochapishwa katika mtandao wa X siku ya Jumanne jioni, Heche aliyekamatwa tangu Oktoba 22 na kuwekwa mahabusu alisafirishwa na polisi siku ya Jumanne kutoka Dodoma hadi jijini Dar es salaam ambako amefunguliwa mashtaka hayo.
CHADEMA imeongeza kuwa Heche alikataa kuandika maelezo yake kwa polisi, akisisitiza kuwa atafanya hivyo baada ya kufikishwa mahakamani. Haijajulikana hasa ni lini atafikishwa mahakamani.
Wafuatiliaji wakosoa hali ya mambo Tanzania
Kufunguliwa kwa mashtaka dhidi ya kiongozi huyo wa upinzani kunajiri baada ya vurugu kubwa kuripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini humo siku ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi kwa asilimia 98 ya kura, kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi. Hata hivyo, upinzani uliutaja uchaguzi huo kuwa "ni maigizo”.
Serikali ilijibu maandamano hayo kwa kuzima kabisa intaneti na kusitisha usafiri wa ndani, hatua iliyofanya iwe vigumu kupata taarifa sahihi kuhusu matukio yaliyokuwa yanaendelea katika taifa hilo la Afrika mashariki.
CHADEMA inadai kuwa mamia ya watu waliuawa na vyombo vya usalama, ingawa idadi kamili haijathibitishwa na serikali.
Mashirika ya haki za binadamu yameelezea ukandamizaji mkali dhidi ya wapinzani kabla ya uchaguzi huo, ambapo viongozi kadhaa wa upinzani walikamatwa au kuzuiwa kimfumo kugombea.
Kiongozi mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu, naye pia hivi sasa anakabiliwa na kesi ya uhaini, kosa ambalo linaweza kupelekea adhabu ya kifo iwapo atapatikana na hatia.