1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chadema yaitaka polisi kutoa taarifa kuhusu Mdude

9 Mei 2019

Chama kikuu cha upinzani Tanzania, CHADEMA kimelitaka jeshi la polisi kuharakisha kutoa taarifa za awali juu ya tukio linalotajwa la kutekwa kwa mwananchama wake Mdude Nyagali.

Tansania Polizeizentrale in Dar es Salaam
Picha: DW/Said Khamis

CHADEMA imeyasema hayo mbele ya wanahabari baada ya kupatikana kwa mwanachama wake aliyetajwa kutekwa ofisini kwake mwishoni mwa juma lililopita na kisha kupatikana usiku wa kuamkia leo akiwa na majeraha katika mwili wake yanayosadikika yanatokana na kuteswa. Mdude amekuwa akijipambanua kama mkosoaji mkubwa wa serikali ya awamu ya tano.

Mkurugenzi wa itifaki na mambo ya nje ya chama hicho, John Mrema, amewaambia wanahababri kuwa viongozi mbalimbali wa jeshi la polisi wamefanya mahojiano na mwananchama huyo licha mahojiano yao kuingiliwa mara kadhaa na madaktari ambao walikuwa wanapambania uhai wake.

Pamoja na mahojiano hayo, Mrema anasema, jeshi la polisi linapaswa kutoa taarifa za awali mapema iwezekanavyo ili kuondoa suintofahamu kwa umma kutokana na tukio hilo na endapo hawatafanya hivyo chama hicho kitaweka wazi mahojiano ya awali jeshi la polisi lililofanya na mwanachama wake huyo.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dr. Vincent Mashinji Picha: Said Khamis

Harakati zilizofanywa mitandaoni na watu mbalimbali zikipinga vikali tukio hilo linalotajwa la utekaji wa mwanachama huyoaliyejipapambanuwa kuikosoa serikali iliyoko madarakani tangu mwaka 2016 zinatajwa kuleta tija katika matukio yanayoshuhudiwa ya utekwaji, uteswaji na mauaji dhidi ya raia, hivyo nguvu hiyo ya umma inapaswa kutumika bila kujali itikadi za kisiasa na kidini kwa kila mmoja.

Kidole bado chanyooshwa

Hata hivyo, bado wanaharakati mtandaoni wanainyooshea kidole mamlaka dhidi ya wanaotoa maoni yao yanayoonekana yapo kinyume na matakwa ya serikali kuwa matatani, ambapo mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi anaigeukia serikali na kutaka kufuata sheria dhidi ya wanaobainika kuwa wanakwenda kinyume dhidi ya sheria.

Mpaluka Saidi Nyangali, ama Mdude Chadema kama anavyojulikana na wengi, mara kadhaa amejikuta akiwa mikononi mwa jeshi la polisi kutokana na mitazamo yake dhidi ya serikali na aliwahi kufunguliwa kesi ya kuchapisha taarifa za uongo katika mitandao yake ya kijamii na uchochezi, kesi ambazo alishinda kutokana na serikali kushindwa kuthibitisha tuhuma hizo.

Pia yeye amelishtaki jeshi la polisi katika Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora na pia serikali katika Mahakama Kuu kanda ya Mbeya akiidai serikali fidia kutokana na madhila ya mateso aliyokuwa akifanyiwa akiwa mikononi mwa polisi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW