CHADEMA yakataa matokeo ya uchaguzi mkuu Tanzania
2 Novemba 2025
Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema kimeyakataa matokeo yaliyompa ushindi wa kishindo Rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi uliosababisha maandamano na vurugu katika maeneo mengi ya taifa hilo la Afrika Mashariki.
Chama hicho ambacho hakikushiriki uchaguzi huo baada ya kukataa kusaini kanuni za uchaguzi na ambacho kiongozi wake Tundu Lissu yuko gerezani tangu mwezi Aprili kwa tuhuma za uhaini, kimesema kwamba matokeo yaliyotangazwa na tume ni ya kutengenezwa.
Chadema imeongeza kwamba hata maandamano yanayoendelea nchini humo yanaonyesha wazi kwamba wananchi hawakushiriki katika zoezi hilo na kwamba wanamkataa yeyote anayetokana na matokeo hayo ya uchaguzi wenye dosari.
Hapo jana, Tume huru ya Uchaguzi Tanzania INEC ilimtangaza Samia mgombea urais kwa tiketi ya chama tawala CCM kushinda katika uchaguzi huo kwa asilimia 98.