CHADEMA yakataa ushindi wa Samia Suluhu
2 Novemba 2025
Baada ya hapo jana Jumamosi Rais Samia Suluhu Hassan kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais nchini Tanzania uliogubikwa na machafuko na maandamano, chama kikuu cha upinzani CHADEMA kimeupinga ushindi huo wa kishindo uliotangazwa na tume.
Chama hicho ambacho kilizuiwa kushiriki uchaguzi baada ya kukataa kusaini kanuni za uchaguzi na ambacho kiongozi wake Tundu Lissu alikamatwa kwa tuhuma za uhaini, kimesema jana usiku kwamba matokeo yaliyotangazwa na tume ni ya kutengenezwa.
Kwenye ukurasa wake wa X chama hicho kiliandika ujumbe huu ''Chadema kinapinga vikali kile kilichoitwa matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na tume ya kitaifa ya uchaguzi. Matokeo hayo hayana msingi wa kiuhalisia kwasababu ukweli ni kwamba hakuna uchaguzi wa kweli uliofanyika nchini Tanzania''
Chama hicho pia kilitaja juu ya hali inayoendelea nchini Tanzania kufuatia uchaguzi huo kwa kuandika ujumbe unaosema '' Maandamano ya nchi nzima ni ishara ya wazi kwamba raia hawakushiriki katika kile kinachoitwa uchaguzi na kwahivyo wanamkataa yeyote aliyetokana na mchakato huu wa uchaguzi wa udanganyifu''
Baada ya ujumbe wa chama hicho kikuu cha upinzani, hakuna tamko lililotolewa mara moja kutoka upande wa serikali.
Baadhi ya waandamanaji waliharibu na kung'oa mabango ya picha ya Samia Suluhu Hassan na kuchoma moto majengo ya serikali huku polisi wakitumia mabomu ya machozi dhidi ya waandamanaji hao na kuwafyetulia risasi, kwa mujibu wa mashahidi wa maandamano yaliyozuka Jumatano siku ya uchaguzi wa rais na bunge.
Mauaji na kilio cha waandamanaji
Mnamo siku ya Ijumaa CHADEMA ilisema mamia ya watu wameuwawa kwenye maandamano huku ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ikisema inazo ripoti za kuaminika zinazoonesha takriban watu 10 wameuwawa kwenye miji mitatu ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Kimsingi waandamanaji wamekasirishwa na hatua ya tume ya uchaguzi ya kuzuia wapinzani wakuu wawili wa Samia Suluhu kuingia katika kinyang'anyiro cha urais na pia kile ambacho mashirika ya kutetea haki za binadamu yamesema ni matukio yaliyoenea ya kukamatwa na kutekwa kwa wapinzani wa serikali.
Serikali imekanusha kuhusu idadi ya vifo iliyotolewa na upinzani ikisema idadi hiyo ''imetiwa chumvi'' na imepinga pia ukosoaji unaotolewa dhidi ya rikodi yake ya haki za binadamu.
Shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha kuhusu idadi ya waliouwawa nchini Tanzania.
Suluhu akemea vitendo vya waandamanaji
Jumamosi baada ya kutangazwa mshindi na kukabidhiwa cheti chake cha ushindi,mjini Dodoma, Samia Suluhu Hassan alikemea vitendo vya waandamanaji akisema ''Havikuwa vya uwajibikaji wala vya kizalendo'' Kwenye hotuba yake pia aliweka wazi kwamba linapohusika suala la usalama wa Tanzania, hakuna mjadala na kwamba wanapaswa kutumia njia zote kuhakikisha nchi inabakia kuwa salama.
Mamlaka za nchi hiyo zilitangaza amri ya watu kutotoka nje nchi nzima tangu siku ya Jumatano na kuzima pia huduma za mtandao wa Internet.
Safari nyingi za ndege zimefutwa na shughuli zimevurugika katika bandari ya Daresalam, kituo kinachotumika kwa uingizaji mafuta na usafirishaji wa bidhaa za chuma zinazochimbwa katika kanda nzima.