1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CHADEMA yalia na kamatakamata ya viongozi

17 Julai 2017

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema kimelaani vikali hatua ya kuendelea kukamatwa kwa viongozi wake kikisema kuwa mwenendo huo unadumaza demokrasia na kukiuka katiba ya nchi.

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Vincent Mashinji
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Vincent MashinjiPicha: Said Khamis

Chama hicho ambacho kinashuhudia viongozi wake wakiangukia mikononi mwa dola mara kwa mara kimesema pamoja na hali hiyo bado hakijavunjika moyo na kitaendelea na harakati zake za kisiasa kote nchini.

Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu aliwaambia waandishi wa habari kuwa kile kinachofanyika sasa ni ukiukwaji wa sheria zinazoruhusu uhuru vyama vya siasa na kwa maana hiyo wataendelea kupaza sauti kukemea tabia hiyo.

Alisema hakuna mwanasiasa ndani ya chama hicho ambaye hajaguswa na mkono wa jeshi la polisi ambalo limekuwa likiwakamata viongozi na kuwashikilia kwa muda katika kile kinachoelezwa ni utekelezaji wa maagizo kutoka juu.

Kuwashitaki viongozi binafasi

Kutokana na hali hiyo, Lissu amedai kuwa kuanzia sasa viongozi wa serikali wanatoa maagizo kukamata wanasiasa hao, watachukuliwa hatua kwa kufikishwa mahakamani. "Na tunamfungulia yeye pekee yake, hatutaki ugonvi na serikali," alisema Lissu katika mkutano na waandishi habari jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe.Picha: DW/H. Bihoga

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mfululizo wa matukio ya kutiwa mbaroni kwa viongozi wa chama hicho kutokana na maagizo yanayotolewa na wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa. Hali hiyo imezusha mjadala mkubwa nchini huku baadhi ya makundi ya wasomi pamoja na wanaharakati wakiwaonya watendaji hao wa serikali juu ya matumizi mabaya ya madaraka.

Ama baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanavitaja vyama vya upinzani kuanza kuangalia upenyo mpya wa uendeshwaji wa siasa zao kutokana na mazingira wanayokumbana nayo. Loisi Kolumba, mmoja ya wale wanaofutilia kwa karibu hali ya kisiasa ya wakati huu, amevishauri vyama hivyo kutafuta mbinu mpya za kufanya siasa kwa kuwa wataendelea kubanwa.

CHADEMA yadai CCM inatumia rishwa kuvutia viongozi wake

Wakati huu mbali ya vuta nikuvute inayoendelea kushuhudiwa kati ya vyombo vya dola na chadema, pia chama hicho katika siku za hivi karibuni kilipata pigo baada ya madiwani wake kadhaa mkoani Arusha kutangaza kuachia ngazi.

Lakini chadema imesema haijashangazwa na kitendo hicho kwa vile inahisi kuwepo kwa kile ilichokiita mchezo mchafu. "Mmoja wa hao madiwani alijiuzulu, haijapita wiki, ameteuliwa kuwa mchumi wa Halmashauri ya wilaya ya Aremeru," alisema Lissu na kusistiza kuwa kilichotokea ni rushwa iliotembea.

Mwishoni mwa wiki, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama tawala CCM, Humprey Polepole aliuambia mkusanyiko mmoja wa chama chake kuwa wako mbioni kuvuna viongozi wengine wa Chadema ndani ya juma hili.

Mwandishi: George Njogopa

Mhariri: Saumu Yusuf

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW