1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CHADEMA yampitisha Lissu kupambana na Magufuli uchaguzi 2020

4 Agosti 2020

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, kimempitisha Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, kuwania urais na hivyo kufunguwa njia kwa mahasimu wawili wakubwa kuchuwana kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 28.

Tansania Dar es Salaam | Politiker | Tundu Lissu
Picha: DW/S. Khamis

Wajumbe 405 kati ya 442 wa Baraza Kuu la chama hicho, jioni ya jana (Agosti 3) walimpitisha Lissu, mwenye umri wa miaka 52, na ambaye ni mwanasheria kitaaluma, kukiwakilisha chama chao kwenye uchaguzi huo unaotazamiwa kuwa na msisimko mkubwa, hasa kwa kuwa Lissu amekuwa mpinzani mkuu wa Rais John Magufuli, aliyeteuliwa na chama chake cha Mapinduzi (CCM) kutetea kiti chake kwa muhula wa pili. 

Lissu, aliyeingia rasmi kwenye siasa za majukwaani mwaka 2010 alipowania na kushinda ubunge wa Singida Mashariki kupitia upinzani, alikuwa anachuwana na Lazaro Nyalandu, waziri wa zamani wa serikali ya CCM aliyehamia upinzani, ambaye amepata kura 36 na mwanamke pekee kujitokeza kuwania nafasi hiyo miongoni mwa watia nia hadi sasa, Dk. Maryrose Majinge, aliyeambulia kura moja. 

Salim Mwalimu amepitishwa kuwa mgombea mwenza wa Tundu Lissu.Picha: DW/M. Khelef

Kwa upande wa Zanzibar, CHADEMA imemteuwa makamo mwenyekiti wake wa huko, Said Issa, kuwania nafasi ya urais, ingawa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, aliuambia mkutano wa Baraza Kuu kuwa wamo kwenye mazungumzo na wenzao wa chama cha ACT Wazalendo juu ya uwezekano wa kushirikiana.

Endapo vyama hivyo vitashirikiana kama ilivyotokea kwenye uchaguzi wa 2015 kati ya CHADEMA, CUF, NCCR-Maguezi na NLD, huenda Maalim Seif Sharif Hamad kutokea ACT-Wazalendo akawa mgombea wao wa pamoja. Maalim Seif amewania nafasi hiyo tangu kurejea tena kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 kupitia, na hii itakuwa mara yake ya sita, na yumkini ya mwisho.

CHADEMA pia imempitisha naibu katibu mkuu wake kwa upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu, kuwa mgombea mwenza wa Tundu Lissu. Mwalimu, mwanahabari kijana aliyeingia kwenye siasa za upinzani mwaka 2010, pia amewahi kuwania mara mbili nafasi ya ubunge kupitia chama chake bila mafanikio.